Mshindi wa kwanza upande wa mitindo kwenye shindano la Redd's Uni fashion Bash, Victor Kashmiry wa Ustawi wa Jamii akipokea shilingi laki saba toka kwa Redd's Miss Tanzania 2013, Hapiness Watimanywa.
|
Na Mwandishi Wetu
FUNGA KAZI! Baada ya Mwanza, Kiliomanjaro na Iringa kusaka washindi wao, kazi ilimalizika juzi usiku pale Dar es Salaam ilipohitimisha tamasha hilo la wanamitindo na wabunifu walio katika vyuo vikuu ndani ya mkoa huo, walipochuana katika shindano la ‘Redd’s Uni-Fashion Bash’, lililofanyika Ukumbi wa Kijiji cha Makumbusho uliopo Kijitonyama.
Ilionyesha dhahiri ushindani ulivyokuwa mkubwa hasa kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ustawi wa Jamii, Taasisi ya Uhasibu (TIA), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Biashara (CBE) na Mwalimu Nyerere.
Kwa upande wa wanamitindo Victor M. Victor kutoka Ustawi wa Jamii alifanikiwa kutwaa nafasi ya kwanza na kujipatia Sh 500,000 huku wa pili akiwa ni Maria wa UDSM aliyeondoka na Sh 400,000 wakati watatu alikuwa Sammy wa UDSM pia aliyepata Sh 300,000.
Kazi ngumu ilikuwa kwa upande wa wabunifu ambapo kulikuwa na ushindani mkubwa zaidi lakini Joachim Kilongoko wa CBE aliondoka na Sh 700,000 wa pili akiwa ni Sarah kutoka UDSM aliyepata Sh 500,000 huku watatu akiwa ni John wa Ustawi wa Jamii aliyejiondokea na na Sh 300,000.
Mbali na hilo watu waliohudhuria pia walipata burudani kali kutoka kwa wasanii wakali hapa nchini Ben Pol na Young Dee waliowapagawisha mashabiki vilivyo.
Washindi wote hao walikabidhiwa zawadi hizo na Redd’s Miss Tanzania, Happiness Watimanywa ambaye alisema amefurahishwa mno na vipaji alivyovishuhudia hapo.
Akizungumza ukumbini hapo, Meneja wa Redd’s kinywaji kinachozaliwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Victoria Kimaro alisema, waliamua kudhamini shindano hilo kwa lengo la kuibua vipaji vya wabunifu na wanamitindo waliopo vyuoni.
Alisema, wanafunzi wa vyuo vyote vya elimu ya juu walio na mapenzi katika ubunifu na mitindo walishiriki shindano hilo, huku akiamini kwa kiasi kikubwa lengo lao limefanikiwa.
Kinywaji cha Redd’s Original pia ndicho kinachodhamini shindano la Redd’s Miss Tanzania na kinazalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
No comments:
Post a Comment