Na Mwandishi Wetu
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu (HESLB) imeongeza muda wa waombaji mikopo kwa mwaka wa masomo
2015/2016 kuwasilisha maombi yao hadi mwishoni mwa mwezi huu (31 Julai, 2015).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa
leo (Jumatano, Julai 15, 2015) na Mkurugenzi Mtendaji wa (HESLB) Bw. George
Nyatega (pichani), hatua hiyo imechukuliwa ili kuwapa fursa wombaji ambao
hawajakamilisha kufanya hivyo.
“Hatua hii imechukuliwa ili kuwapa
fursa wale ambao kwa sababu mbalimbali hawakuweza kufanya maombi ya mikopo
katika muda uliopangwa,” amesema Bw.
Nyatega katika taarifa yake iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari.
Itakumbukwa kuwa awali Bodi ilianza
kupokea maombi kwa njia ya mtandao (www.olas.heslb.go.tz)
tarehe 4 Mei, 2015 na mwisho wa kuwasilisha maombi ulipangwa kuwa tarehe 30
Juni, 2015.
Kupitia taarifa yake, HESLB
imewataka waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2015/2016 ambao
hawajakamilisha maombi yao kukamilisha na kuwasilisha maombi yao ya mikopo
ndani ya muda ulioongezwa na kusisitiza
kuwa hakutakuwa na muda mwingine wa nyongeza baada ya tarehe 31 Julai, 2015.
HESLB
ilianzishwa kwa sheria ya Bunge na 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai,
2005 ili, pamoja na majukumu mengine kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji
waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu.
No comments:
Post a Comment