Kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola hapa nchini, kwa ushirikiano na TAMISEMI, imefanya uzinduzi wa mashindano ya umoja wa shule za sekondari (Umisseta) kwa kanda ya Kaskazini, mkoani Arusha kwa kugawa vifaa vya michezo kwa shule mbalimbali za sekondari za serikali na binafsi.
Katika uzinduzi wa mashindano hayo jijini Arusha, kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mwishoni mwa wiki, mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa mkoa wa Arusha - Mrisho Gambo, ambapo aliishukuru kampuni ya Coca cola kwa udhamini kufanikisha michuano yam waka huu.
Kwa upande wake, Meneja Mauzo wa Coca-Cola mkoa wa Arusha, Boniface Mwasi alisema kuwa kampuni hiyo imeona umuhimu wa kuibua vipaji vya michezo ndio maana wamejikita kufadhili michezo kama hiyo kwa vijana.
“Tumeamua kushirikiana na serikali katika michezo hii ya Umisseta lengo letu kubwa likiwa ni kuibua vipaji vingi vya michezo kwa kuwa tunaamini mtandao wa shule za sekondari ni mkubwa na ni rahisi kuibua vipaji vingi kutoka sehemu zote za nchi”, Alisema Mwasi.
Aidha, aliongeza ya kwamba kampuni ya Coca-Cola itaendelea kuunga mkono jitihaa za serikali za kukuza sekta ya michezo nchini hususani katika ngazi za chini ambako imekuwa ni vigumu kupata ufadhili kwa kuwa tunaamini kuwa vipaji vinapaswa kuibuliwa na kukuzwa.
“Tunayo dhamira kuona vijana wa kitanzania walioibukia kwenye mashindano haya wanafika mbali kimichezo”, Alisisitiza Mwasi.
No comments:
Post a Comment