Tangazo

September 30, 2011

Jeshi la Serikali ya Mpito Libya latwaa Uwanja wa Ndege, Sirte

Picha za Gaddafi zang'olewa uwanjani hapo.
Wanajeshi wanaoitii serikali ya mpito ya Libya wametwaa uwanja wa ndege katika mji wa Sirte, mahali alikozaliwa aliyekuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi.

Wapiganaji walisonga mbele kupitia majengo ya uwanja wa ndege yaliyoharibiwa, wakiharibu miundombinu ambayo ilikuwa alama ya utawala wa Gaddafi.

Taarifa kuhusu alipo kiongozi huyo wa Libya, aliyeng'olewa madarakani, bado haijulikani lakini wengi wa wanafamilia wake wamekwisha kimbia kutoka Libya.

Mtoto wake wa kiume Saadi yuko nchini Niger. Saa kadha baada ya hati ya kumkamata kutolewa, waziri mkuu wa Niger amesema Saadi hatarejeshwa nchini Libya.

Taarifa ya Shirika la Polisi la Kimataifa, Interpol, ya kukamatwa kwa Saadi Gaddafi, inasema anatakiwa nchini Libya ambako anatuhumiwa kujipatia mali kimabavu na kutumia vitisho vya kijeshi wakati alipokuwa kiongozi wa Shirikisho la Kandanda la Libya.

Interpol imesema akiwa kamanda wa vikosi vya kijeshi, anatuhumiwa kuhusika katika ghasia dhidi ya raia wakati wa maasi, pia anakabiliwa na vikwazo vya Umoja wa Mataifa, vikiwezo vya usafiri na kukamatwa mali zake.

Interpol imesema Saadi kwa mara ya mwisho alionekana nchini Niger na kuziomba nchi wanachama kusaidia kubaini alipo na kumrejesha Libya.

Lakini akizungumza nchini Ufaransa, Waziri Mkuu wa Niger Brigi Rafini amesema Saadi Gaddafi uko salama na "yuko katika mikono ya serikali ya Niger" katika mji mkuu Niamey.

"Kwa sasa, hakuna suala la yeye kupelekwa Libya" Bwana Rafini ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP, akisema hatatendewa haki ya kimahakama akipelekwa huko.

Interpol tayari imetoa hati ya kukamatwa kwa Kanali Gaddafi na mtoto wake mwingine wa kiume, Saif al-Islam.

Wapiganaji watiifu kwa Gaddafi wamekuwa wakiweka upinzani mkali katika mji wa Sirte tangu askari wanaowaunga mkono wapiganaji wa Baraza la Taifa la Mpito la Libya (NTC) waanze mashambulio yao katika mji huo.

Majengo mawili ya viongozi Mashuhuri katika uwanja wa ndege wa Sirte ni ya kifahari, yakidhihirisha mji wa nyumbani kwa Muammar Gaddafi - yakiwa yamewekewa skrini kubwa za Televisheni, bafu ya mvuke au Sauna na kitanda kikubwa.

Wapiganaji vijana waliegesha bunduki zao katika viti vilivyonakishiwa kwa dhahabu, wakitaniana na kufurahia madaraka ya ghafla waliyoyapata - wachache kati yao wamewahi kuuona mji wa Sirte hapo kabla, achilia mbali mazingira ya kifahari aliyoishi kiongozi wao.
Uharibifu

Malori yaliyochorwa chorwa rangi yaliharibiwa katika barabara ya lami, wakilenga ngome ya majeshi ya Gaddafi katika upande wa pili wa barabara ya kurukia na kutua ndege.

Wiki mbili zilizopita, majeshi ya NTC yaliutwaa uwanja wa ndege, umbali mfupi kutoka katikati ya mji, lakini wakarudishwa nyuma na wanajeshi wanaomtii Gaddafi.

Mwandishi wa BBC, Jonathan Head anasema wakati huu majeshi ya NTC yana matumaini ya kuutwaa kabisa uwanja huo wa ndege, mbali na kukabiliwa na mashambulio ya maroketi na bunduki kutoka upande wa pili wa njia ya kurukia na kutua ndege.

Uwanja wa ndege upo umbali wa kilomita 5 (maili 3) kutoka mjini Sirte.

Majeshi ya Baraza la Mpito la Taifa la Libya (NTC) hivi karibuni pia yalitwaa bandari ya Sirte.
Makabiliano makali

Mapigano makali yameripotiwa kuendelea Alhamisi, kwa pande zote mbili wakishambuliana kwa silaha nzito za kivita.

Ndege za Nato zimekuwa zikiendesha mashambulio ya anga dhidi ya vituo vya kijeshi yakiwemo maghala ya kuhifadhi silaha na risasi.

Miji ya Sirte na Bani Walid ni maeneo makubwa ya mwisho ambayo yako chini ya udhibiti wa wafuasi wa Gaddafi, na miji yote miwili imeshuhudia mapigano makali katika siku za karibuni.
Gaddafi na familia

Maafisa wa NTC wanasema wanaamini kuwa Kanali Gaddafi huenda anajificha katika jangwa kusini mwa Libya.

Wanasema mmoja wa watoto wake wa kiume, Mutassim, huenda yuko Sirte, na mwingine, Saif al-Islam, yuko Bani Walid.

Mke wa Kanali Gaddafi na watoto wake watatu walikimbilia Algeria mwezi uliopita. Na watu wengine wa familia ya Gaddafi walikwenda Niger.
Source: BBC Swahili

No comments: