TIMU ya Taifa ya Soka ya Zanzibar, Zanzibar Heroes inatarajiwa kuondoka nchini Novemba 7 mwaka huu kuelekea nchini Misri kufanya majaribio ya mechi za kimataifa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya timu hiyo kwa mashindano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) Safari hiyo ilimewezeshwa kwa ushirikiano kati ya kampuni ya Future Century Ltd, Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) na Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo ya Zanzibar.
Taarifa kwa vyombo vya habari ikimnukuu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Future Century, Hellene Masanja imesema, timu hiyo ya soka ya Visiwani Zanzibar itakaa nchini Misri ikijipima nguvu kwa kucheza za timu mbalimbali nchini humo kutoka Tarehe 9 Novemba hadi 21 Novemba mwaka huu.
Ikiwa nchini Misri siku ya Tarehe 9 Novemba, Heroes itakwaana na timu ya Suez Canal katika mechi itakayochezwa kwenye uwanja wa timu hiyo, ambapo Novemba 11 itachuana na na timu ya NDP ikifuatia mchuano mwingine dhidi ya timu kali ya Arab Contractor hapo Novemba 14.
Kikosi hicho cha timu ya soka ya Zanzibar kinachonolewa na kocha Stewart Hall raia wa Uingereza kitashuka tena dimbani Novemba 16 kuonyeshana kazi na timu ya Vijana chini ya umri wa miaka 23 katika Uwanja wa timu ya Taifaya nchi hiyo na kufanya tena mechi ya marudiano Novemba 18 kabla ya mechi yao ya mwisho dhidi ya timu ya Al Canal Novemba 20 timu ya soka iliyomnunua mchezaji kuitoka Zanzibar, Ali Badri.
Mofisa watakaoambatana na timu hiyo kwenda Misri ni Sada Salum wa Baraza la Michezo Zanzibar (ZCS), Katibu Mkuu wa ZFA, Masoud Attai, kocha msaidizi, Hemed Moroco, Ofisa Habari wa ZFA, Munir Zakaria huku kocha wa timu hiyo, Stewart Hall akiondoka nchini Novemba 10 wakati wachezaji wa timu hiyo waliomo katika timu ya Taifa Stars,Nadir Haroub Canavaro, Muadini Ali Muadini, Aggrey Morris na Nasoro Masoud wao watajiunga na Heroes nchini Misri Novemba 16.
Safari hii ya Zanzibar Heroes ni moja ya matunda ya hafla ya kuichangia timu hiyo iliyoandaliwa na Future Century Ltd, ZFA na Wizara ya Habari, Utalii,Utamaduni na Michezo ya visiwani humo iliyofanyika Machi 26 mwaka huu mjini Zanzibar mgeni rasmi akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein ambaye pia ni mlezi wa timu hiyo.
Katika hafla hiyo kiasi cha shs 86,841,000/- zilichangwa kwa njia michango na ahadi japo hadi sasa ni kiasi cha shs 59,841,000/- ndizo zilizopatikana.
Timu ya Azam iliahidi kutoa shs 5,000,000; United Petroleum shs 5,000,000; Carl Salisbury wa ZanAir shs 6,000,000; Shirika la Bandari Zanzibar USD 4,000,000; Benki ya Watu wa Zanzibar USD 4,000,000; Abubakar Bakhresa wa timu ya Azam alinunua jezi iliyosainiwa na Rais Shein kwa shs 1,000,000; jezi iliyosainiwa na Zanzibar Heroes ilinunuliwa na ZPC kwa shs 2,000,000; PVR decoder iliyotolewa na Multichoice ilinunuliwa na PBZ kwa shs 2,000,000; kampuni ya Affordable Housing ikitoa kamera ambayo iliinunua tena kwa USD 500 huku picha mbili za Rais wa Zanzibar zilinunuliwa na Zanzibar Beach Resort na ZPC KWA SHS 8,000,000/-.
Hafla hiyo ya uchangiaji ilifanikiwa chini ya udhamini wa Zan Air, ZPC, PBZ, Shirika la Bima Zanzibar, SuperSports Africa, Multi-Choice Tanzania, Kampuni ya Konyagi (TDL) , United Petroleum, Zantel, Zanzibar Beach Resort, General Agency Limited, Hoteli ya New Africa, Affordable Housing, Explore Zanzibar na Vayle Springs Limited.
No comments:
Post a Comment