RPC Dodoma, SACP Zelothe Steven |
Luppy Kung’alo na Silyvester Onesmo wa Jeshi la Polisi Dodoma
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la RICHARD NGALYA mwenye umri wa miaka 33, Mkazi wa Mpunguzi katika Manispaa ya Dodoma, Mkulima anayetuhumiwa kuwa mwizi maarufu wa Mifugo ameuawa na wananchi wenye hasira kali baada ya kukutwa akitaka kuiba Ng’ombe katika Zizi.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dododma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Bw. Zelothe Steven alisema tukio hilo lilitokea siku ya Jumatatu majira ya saa nane usiku ambapo mwizi huyo alikutwa katika Zizi la Ng’ombe mali ya Bw. YOHANA MAN’GONDA miaka (89) akilifungua kwa lengo la kuiba ng’ombe.
Kamanda Zelothe Steven alisema marehemu alikutwa na watoto wawili wa Mzee mwenye zizi hilo, ambaye aliwaagiza watoto wake kulilinda baada ya siku moja kabla ya tukio la kuuwawa, marehemu alikutwa na vijana hao katika jitihada za kutaka kulifungua zizi hilo.
Hivyo siku ya tukio watoto hao, wakiwa katika ulinzi, ndipo walipomkuta mwizi huyo wa mifugo na kupiga yowe, ambapo majirani na watu wengine wakaribu wakatoka na kumfukuza hadi katika mlango wa nyumbani na mwizi huyo ambapo walimshushia kipigo kikali.
“Baada ya Kumpa kipigo hicho walimkamata na kumpeleka kwa viongozi wa kijiji hicho cha Mpunguzi, ambapo alipofikishwa katika ofisi za kijiji alifariki dunia” aliongeza Kamanda Zelothe Steven.
Hata hivyo Kamanda huyo wa Polisi Mkoa wa Dodoma, alikemea vikali hatua na vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mikononi , na kusema kuwa kinyume kabisa na haki za msingi za binadamu pamoja na sheria za nchi kwa ujumla.
Aidha aliwataka wananchi kutekeleza dhana nzima ya utii wa sheria bila shuruti, inayotaka mwananchi kutekeleza sheria pasipo matumizi ya nguvu zinazoweza kuleta madhara kwa binadamu kutumika.
Aliwataka wananchi hao kuacha kujichukulia sheria mikononi na kutoa wito kwao wa kutoa taarifa katika vituo vya Polisi vilivyo jirani mara matukio ya uhalifu yanapotokea katika maeneo yao ili hatua za msingi za kutekeleza sheria zifuatwe.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kwa wanakijiji hicho, walidai mwizi huyo alikuwa mzoefu na kwamba alishawahi kufungwa kwa kosa la wizi wa mifugo, ambapo alihukumiwa miaka thelathini (30) jela ambapo alitumikia miaka nane na kutoka kwa rufaa mwaka jana.
No comments:
Post a Comment