Tangazo

April 25, 2012

Watu Wawili wamefariki Dunia Mkoani Dodoma: Mmoja atwangwa Mchi kichwani na Mkewe

Katika tukio la kwanza limetokea mnamo tarehe 24/04/2012 majira ya saa 23:00 usiku maeneo ya Kikuyu Manispaa ya Dodoma ambapo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la ZACHARIA S/O SADALA mwenye umri wa miaka 37, mbeba mizigo, mkazi wa Kikuyu. 

Mtu huyu aliuawa kwa kupigwa na mchi kichwani na kuchomwa na kisu shingoni karibu na kolomeo, alipigwa   na mke wake aliyetambulika kwa jina la JENIFER D/O JOHN mwenye umri wa miaka 37, Mkristo, Mkulima na  Mkazi wa Kikuyu.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi wa kifamilia, kwani marehemu na mke wake walikuwa na tabia ya kutukanana na kugombana mara kwa mara, hivyo siku ya tukio walianza kutukanana na hatimaye kupigana na kusababisha mauaji.
 
Mtuhumiwa amekamatwa na anashikiliwa na Jeshi la Polisi na atafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.
 
Aidha katika tukio la pili ambalo ni la ajali ya gari limetokea tarehe 24/04/2012 majira ya saa kumi na nusu 16:30 jioni katika maeneo ya Mpunguzi Kata ya Mpunguzi Manispaa na Mkoa wa Dodoma katika  barabara kuu ya Dodoma/Iringa.
 
Ambayo ilihusisha Basi la abiria  lenye namba za usajiri T. 627 BBD Leyland Bus Mali ya Kampuni ya WOSIA WA MAMA, lilimgonga mtembea kwa miguu aliyetambulika kwa jina la JOHN S/O PETER mwenye umri wa miaka 33, Mkulima, mkazi wa Mpunguzi na kusababisha kifo chake papo hapo.
 
Basi hilo  lilikuwa likiendeshwa na Dereva  DAUDI S/O KILIMOKA mwenye umri wa miaka 44, Mkazi wa Mpunguzi, ambaye amekamatwa, basi hilo lilikuwa  likitokea Dodoma Mjini kuelekea Vijijini kwenye Kijiji cha Manzase.
 
Katika tukio hili marehemu, ambaye ni mfanyabiashara alikuwa  ameuza mzigo wake na akiwa bado hajalipwa fedha ya mzigo aliokuwa ameuza hivyo alining’inia mlangoni karibu na kwa dereva ili aweze kumuona mtu aliyemuuzia mzigo wake na aweze kulipwa fedha zake.
 
Hivyo basi  dereva aliamua kuondoa gari kwa ghafla na mara marehemu akateleza na kuangukia chini ya uvungu wa gari na kukanyagwa na tairi za gari na kusababisha kifo chake papo hapo.
 
Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kuendesha gari wakati akimuona mfanyabiashara huyo  akiwa amening’inia mlangoni.
 
Wito unatolewa kwa Madereva kufuata sheria za usalama Bara barani ili kuepuka ajali zisizo za lazima.

Imetolewa na:
 ZELOTHE STEPHEN - SACP
KAMANDA WA POLISI MKOA WA DODOMA

No comments: