Dk. Mahanga akizungumza na waandishi wa habari punde baada ya hukumu hiyo. |
Mbunge wa Jimbo la Segerea, Dk. Miltoni Makongoro Mahanga, ameibuka mshindi katika kesi iliyokuwa inamkabili ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010 yaliyompa ushindi.
Kesi hiyo namba 98 ya mwaka 2011 ilifunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo katika jimbo hilo, kupitia Chadema, Fredy Mpendazoe, akipinga matokeo ya uchaguzi huo yaliyompa ushindi Dk Mahanga wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mbali na Dk Mahanga ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, wadaiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG), Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, ambaye ni Msimamizi wa Uchaguizi wa majimbo ya Ilala (mdaiwa wa tatu).
Wakati katika kesi hiyo Mpendazoe amekuwa akiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala, Dk. Mahanga amekuwa akitetewa na Mawakili Jerome Msemwa na Aliko Mwamanenge wakati AG na Mkurugenzi wakitetewa na Mawakili wa Serikali David Kakwaya na Seith Mkemwa.
Katika kesi hiyo, Dk. Mahanga anadaiwa kukamatwa na wananchi Tabata Kimanga akiwa na masanduku ya kura na kisha kukabidhiwa katika kituo cha Polisi Buguruni.
Pia inadaiwa moja ya ukiukwaji uliojitokeza kwenye uchaguzi huo ni pamoja na kutokutangaza matokeo ya kituo kimojakimoja, kuyapatia ufumbuzi matokeo ya vituo mbalimbali yaliyopotea katika kata ya Kiwalani naVingunguti pamoja na kudaiwa kushuhudia masanduku mengine ya kura yakiwa matupu.
Upande wa mashtaka ulifunga ushahidi wake Machi 21 baada ya kuwaita mahakamai jumla ya mashahidi 13 ambao walitoa ushahidi katika kesi hiyo.
Hata hivyo hadi upande wa mashtaka unafunga ushahidi wake haukuweza kuwasilisha mahakamani kielelezo chochote kuwa sehemu ya ushahidi wake, baada ya upande wa utetezi kupinga baadhi ya vielelezo ambavyo Mpendazoe aliyetoa ushahidi wake akiwa shahidi wa kwanza.
Wakati akitoa ushahidi wake, Mpendazoe aliomba mara mbili kuwasilisha mahakamani hapo vielelezo viwili kwa nyakati tofauti ili viweze kuwa sehemu ya utetezi wake lakini akagonga mwamba baada ya mawakili wa upande wa mashtaka kumwekea pingamizi.
Jaji alikubaliana na hoja za utetezi na kuukataa kuwa haujakidhi vigezo vya kuwa nyaraka ya umma.
Katika kesi hiyo , Mpendazoe analalamikia mwenendo mzima wa uchaguzi katika jimbo hilo akidai taratibu na sheria za uchaguzi zilikiukwa.
Hivyo aliiomba Mahakama hiyo itengue ushindi wa Dk. Mahanga na kuamuru ufanyike uchaguzi mdogo, au yeye atangazwe mshindi.
No comments:
Post a Comment