Tangazo

May 18, 2012

NAPE: CCM NDICHO CHAMA PEKEE CHENYE DEMOKRASIA YA KWELI NCHINI

Nape Nnauye
NA MWANDISHI WETU

CCM ndicho chama cha kisiasa chenye demokrasia ya kweli tofauti na vyama vya upinzani vinavyoonekana kujaa udikteta na hivyo kubaki kuwa kama vyama vya harakati tu.

Tofauti na CCM ambayo wanachama wake wana uhuru wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, katika vyama vingine hawapati fursa hiyo kutokana na viongozi wake kuwajia juu wanachama wanapojitokeza kutaka kuwania nafasi za uongozi.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye wakati akifungua Mkutano wa Uchaguzi wa viongozi wa ngazi mbalimbali tawi la CCM, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya Chama mjini Dar es Salaam.

Akifungua mkutano huo katika ukumbi wa Burudani wa Vijana, Kinondoni, Nape alisema, mfano wa karibuni wa vyama vya upinzani kuonyesha kuwa ni vya harakati za watu fulani tu, ni ule wa Chadema kuamua munjia juu mbunge wake wa Maswa, John Shibuda, baada ya kutangaza kugombea Urais uchaguzi mkuu ujao, kwa tiketi ya chama hicho.

Akiwa kwenye semina ya Utawala bora iliyoandakiwa na APRM mjini Dodoma, Shibuda alisema atagombea urais kwa tiketi ya Chadema katika uchaguzi mkuu ujao (2015) na kwamba anamuomba Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kumpigia debe atakapokuwa akigombea nafasi hiyo.

"Ninyi nyote ni mashahidi, mmesikia jinsi Chadema walivyomjia juu Shibuda baada ya kujaribvu kutangaza kutaka urais kwa tiketi ya chama hicho. wanaharakati wa Chadema wameibuka na kumjia juu, lakini sababu kubwa ni kwamba ametangaza nia hiyo huku akiwa yeye hatoki kanda ya Kaskazini", alisema Nape na kuongeza;

"Kama angetangaza nia hiyo mwanaharakati mwenzao kutoka kanda yao, wasingemjia huu... Ndiyo maana nasema kwamba chama cha siasa cha kweli bado ni CCM tu, vingine ni vyama vya harakati ingawa vimesajiliwa kama vyama vya siasa", alisena Nape.

Nape alisema Chadema hawawezi kukwepa kwamba si chama cha harakati kinachopigania kuwagawa Watanzania kwa majimbo na kuwataka Chadema kama wanataka kujisafisha wamkemee hadharani mbunge wao wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari kwa tamko la hivi karibuni linalomtia matatani.

Nape lisisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi bado ni imara, na kuwataka wana-CCM kutembea vufua mbele mitaani na kuachana na kelele za 'wanaharakati' za kuwatisha ili kuonea aibu chama chao.

Kuhusu uchaguzi huo, Nape aliwakumbusha wana-CCM kwamba tamko la CCM kuhusu kuwachukulia hatua wagombea wanaotumia mbinu chafu za rushwa, si utani ni azimio la dhati na atakayethubutu kubainika akikiuka agizo hilo atakuwa wa mfano kwa wengine.

"Halmashauri Kuu ya CCM ilipitisha uamuzi huu kule Dodoma kwa sababu chama kinataka kila mmoja aweze kugombea nafasi yoyote ya uongozi tofauti na mazingira yanayotaka kujengwa na baadhi ya watu yanayotengeneza mazingira ya kuwezesha wenye uwezo tu kupata uongozi", alisema.

Kwa mujibu wa agizo hilo la CCM, mwanachama sasa hataruhusiwa kujipitisha kwa wapigakura au kukutana nao katika vikao vyovyote kwa namna yoyote kabla ya siku ya uchaguzi.

CCM imesema endapo atapatikana mwanachama atakayejihusisha na kadhia hiyo atafungiwa kugombea au kufutiwa matokeo kama ameshinda uchaguzi na pia kupewa adhabu nyingine ya kinidhamu.

Akizungumzia maslahi ya wafanyakazi, Nape aliahidi kupambana katika ngazi husika kuhakikisha mishara ya wafanyakazi wa Chama inaongezeka na pia kuhakikisha CCM inatoa kipaumbele suala la mafunzo kwa wafanyakazi hao na kuingizwa katika mipango maalum ya kupata viwanja vya kujenga vyumba za makazi.

Mbali na Nape mkutano uchaguzi huo umehudhuriwa na viongozi kadhaa wa Makao Makuu ya CCM kama wanachama wa tawi hilo wakiwemo, Katibu wa NEC Oganaizesheni, Asha Abdallah Juma, Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM, Martine Shigella.

Katika uchaguzi huo wagombea uenyekiti ni Asheri Enock, Furaha Henri na Innocent Anthony, huku nafasi ya Katibu ni Rozalia Thomas, Shabani Masenga na Scolastika Salim.

Mwenyekiti wa zamani Venance Mkude hakugombea tena nafasi hiyo baada ya kumaliza kipidi chake kumalizika kutokana na kustaafu kazi Makao Makuu ya CCM.

No comments: