Tangazo

May 8, 2012

UBAKAJI: MADAKTARI WAELEZA JINSI YA KUTUNZA USHAHIDI


Madaktari wamewatahadharisha kwamba mtu anayebakwa  kamwe asioge au kubadilisha nguo kwa sababu kufanya hivyo kunapoteza ushahidi muhimu wa kumtia hatiani kisheria
mtu aliyebaka.

Wamesema mtu akibakwa  anapaswa  kwenda polisi haraka kupata fomu ya PF3  na awahishwe  hospitali ya wilaya  ambako ataweza  kupatiwa matibabu ikiwa ni pamoja  na dawa ya kuzuia maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU)

Dawa ya kuzuia maambukizi ya (VVU) inayojulikana kama PEP inaweza kufanya kazi endapo tu mwathirika atapatiwa ndani ya saa 72 baada ya kubakwa na endapo kabla ya kubakwa alikuwa hana maambukizi.

Dakta, Zuberi Mzige wa hospitali ya  Mwananyamala, katika wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam amesema watoto, wasichana na wanawake wengi wanaofika hospitali baada ya kubakwa wanakuwa wamepoteza ushahidi kutokana na kuoga na kubadili nguo walizokuwa wamevaa wakati wakibakwa.

Aidha amesema wengi waliobakwa wanafika hospitalini wakiwa wamechelewa na hivyo kuwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU.

Amesema kesi nyingi  za ubakaji zimekuwa zikikosa ushahidi wa daktari kwa sababu aliyebakwa anatakiwa kupelekwa hospitalini akiwa vilevile na nguo zake na uchafu ule ule kwa sababu ushahidi wa polisi na daktari ya kuwa umebakwa ni pamoja na nguo ulizobakwa nazo tena bila kuzibadilisha.

Dakta Prisca Berege  anayeshughulika na magonjwa ya watoto katika hospitali ya Mwananyamala amesema kuna tatizo kubwa la ubakaji hasa kwa watoto  Dar es Salaam na kwamba hatua zisipochukuliwa taifa litapata madhara makubwa.

Akizungumza  na  wanahabari  walioshiriki katika utafiti wa  masuala ya ukatili wa kijinsia  uliofanya na TAMWA  wilaya ya  Kinondoni  Dakta Berege amesema  kwa wastani kila siku hospitali hiyo inapokea  watu watatu waliobakwa ambao ni wanawake na watoto.

Dakta  Begere  amesema vitendo vingi vya ubakaji vinaripotiwa hospitalini hapo nyakati za usiku hivyo amewaasa wazazi kuepuka kuwatuma watoto wao usiku.

Aidha amewataadharisha  wasichana kujiepusha kwenda kwenye  nyumba za wanaume hata kama wanawaamini na ni marafiki zao kwani baadhi yao wanaume  wanakuwa na  nia mbaya ya kubaka hata kama ni mchana.

Ametoa mfano wa binti mmoja ambaye hivi karibuni alibakwa mchana kweupe kwenye nyumba ya mwanaume aliyemwamini na kumthamini kama kaka yake na mwajiri wake. Mwanamme huyo alimwita msichana huyo nyumbani kwa kumdanganya kuwa kuna kazi wangekwenda kupanga kufanya.
 
Imetolewa na:
Ananilea Nkya
Mkurugenzi Mtendaji TAMWA

No comments: