Tangazo

June 1, 2012

Waziri amtimua kigogo Bodi ya Pamba

Christopher Chiza
WAZIRI wa Kilimo, Chakula na Ushirika; Mhandisi  Christopher Chiza ameibuka na kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Tanzania, Michael Ntunga aliyekuwa akilalamikiwa kwa siku nyingi na wadau wa zao hilo.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS); Charles Ekelege ili kupisha taratibu za kisheria ikiwamo suala la uchunguzi dhidi yake kufanyika.

 Ekelege anatuhumiwa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Deo Filikunjombe ilimtuhumu Ekelege baada ya kubaini kuwepo kwa udanganyifu kwenye mpango wa TBS wa kukagua bidhaa nje ya nchi.
 
Wakati Waziri Chiza akimsimamisha kazi kigogo huyo wa Bodi ya Pamba, Naibu Waziri wa Nishati, George Simbachawene naye amewashukia watendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco) mkoani Dodoma, akisema baadhi ni wababaishaji.

Chiza alitangaza kumsimamisha mkurugenzi huyo jana nyumbani kwake kwenye Wilaya mpya ya Kakonko Mkoa wa Kigoma alipokuwa kwenye ziara yake ya kutembelea jimbo lake la Uchaguzi la Buyungu.

Alisema amechukua hatua hiyo kupisha uchunguzi wa tuhuma zanazomkabili kigogo huyo na akibainika ana hatia, hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
 
Moja ya tuhuma zinazomkabili mkurugenzi huyo ni kufuja fedha za fidia za wakulima wa pamba zilizotolewa mwaka 2009 na Serikali kwa lengo la kuziba hasara iliyojitokeza kutokana na kuporomoka kwa bei ya zao la pamba katika soko la dunia.
 
Madai mengine yanayomkabili mkurugenzi huyo ni kushindwa kusimamia usambazaji wa dawa ya kuua wadudu waharibifu wa pamba na kwa msimu huu, dawa zilizosambazwa hazina ubora na hivyo zimeshindwa kuua wadudu wa zao hilo.
 
Ntunga anadaiwa pia kupitisha madai ya malipo ya Sh 50milioni kwa Kampuni itakayonunua zao hilo kwa kila kanda hali ambayo ilipingwa na wanunuzi wakidai kuwa ingemkandamiza mkulima wa mwisho, wakati  lengo la kuanzishwa kwa bodi hiyo ni kuinua maisha ya wakulima wa kilimo hicho.

Uamuzi wa Waziri

Kufuatia hali hiyo, Waziri Chiza alisema ameamua mkurugenzi huyo akae pembeni kupisha uchunguzi na tayari amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo amsimamishe kazi mara moja.

Bodi hiyo ilitajwa katika ripoti CAG kwamba imekuwa na matumizi tata ya mabilioni ya fedha hatua ambayo ilimfanya Rais Kikwete alipokuwa akitangaza baraza la mawaziri Ikulu Mei 4, kusema kuwa safari hii Serikali yake itawang'oa hadi watendaji na wenyeviti wa bodi wa mashirika na wizara ambazo zimetajwa. 
George Simbachawene


Simbachawane naye acharuka

Katika hatua nyingine, Simbachawene jana aliwashukia watumishi Tanesco mkoani Dodoma na kuwataka waache ubabaishaji na mazoea kwa kuwa huduma yao bado ni mbovu na kuwataka wasafishe rushwa ndani ya shirika lao.

Simbachawene alisema ndani ya Tanesco kuna watumishi wahuni na wezi ambao pia hawalitakii mema taifa lao na mara nyingi wamekuwa wakiliibia Shirika kwa visingizio lukuki.

Alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Tanesco Kanda ya Dodoma na kuapa kwamba, atakufa kwa kuwatumikia Watanzania kwani hayuko tayari kuporwa nafasi yake kwa uzembe.

Naibu Waziri huyo alisema kwa muda mrefu shirika hilo limekuwa likitoa visingizio vingi na kwamba kwa sehemu kubwa visingizio vyao vinatokana na mazoea ya muda mrefu.

“Tatizo ni ubabaishaji mkubwa ndani ya shirika lenu, mara nyingi mnakuwa na mipango ambayo hata hivyo haitekelezeki na uhuni mwingi. Lazima mfahamu kuwa huo wote ni wizi unaotokea mchana kweupe,’’ alisema Simbachawene na kuongeza;

“Wakati mwingi haingii akilini mtu kuona nguzo moja ya Tanzania inauzwa bei ya chini nchini Kenya wakati hapa tunatumia nguzo kutoka Afrika ya Kusini ambayo ni bei ghali, ndio maana nasema mnatengeneza mianya ya rushwa mchana kweupe.’’

Alishangaa kuona idadi kubwa ya wafanyakazi wa shirika hilo ni watu wa utawala badala ya kuwa na idadi kubwa ya mafundi hali ambayo inasaidia kuzalisha vishoka.
Gazeti la Mwananchi Juni 01.2012

No comments: