Tangazo

October 13, 2012

Tume ya Katiba kukutana na Baraza la Wawakilishi, Wabunge kesho

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba (kushoto) na Katibu wa Tume, Bw. Assaa Rashid katika mkutano na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
 **********************************
Na Mwandishi Wetu,

Kama sehemu ya mkakati wake wa kukutana na wadau mbalimbali, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatarajia kukutana na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar siku ya Jumapili, terehe 14 Oktoba mwaka huu (2012) ili kukusanya maoni yao kuhusu Katiba Mpya.

Mkutano huo kati ya Tume na Wajumbe wa Baraza Wawakilishi utafanyika kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar na unalenga kuwapa fursa wawakilishi hao wa wananchi kutoa maoni yao mbele ya Tume.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari  iliyotolewa leo (Alhamisi, Oktoba 11, 2012) na Katibu wa Tume hiyo Bw. Assaa Rashid, baada ya mkutano huo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba pia itafanya mkutano na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma tarehe 3 Novemba, 2012.

Bw. Rashid amesema pamoja na kukutana na wawakilishi hao wa wananchi, Tume pia imepanga kukutana na vyama vya siasa, taasisi za kidini, asasi za kiraia, vyama vya kitaaluma na wawakilishi wengine wa makundi mbalimbali ya kijamii kwa lengo la kupata maoni yao kuhusu Katiba Mpya.

Hadi mwishoni mwa mwezi uliopita (Septemba, 2012), Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikua imetembelea na kukutana na wananchi wa makundi mbalimbali katika mikoa 15, ambayo ni Tanga, Dodoma, Shinyanga, Kagera, Pwani, Manyara, Kigoma, Kusini Unguja na Kusini Pemba. Mikoa mingine ni Katavi, Mwanza, Mbeya, Ruvuma, Lindi na Morogoro.

Kwa mujibu wa Tume hiyo, katika mikoa hiyo, jumla ya mikutano 842 ilifanyika ambapo wananchi 517,427 walihudhuria. Kati ya hao, wananchi 102,002 walitoa maoni yao kwa maandishi kuhusu Katiba na wananchi 29,514 walitoa maoni yao kwa kuzungumza katika mikutano hiyo.

Hivi sasa Tume inaendelea na awamu tatu ya kukusanya maoni katika mikoa tisa (09) ya Tabora, Rukwa, Singida, Iringa, Njombe, Kilimanjaro, Mtwara, Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba. Awamu hii inatarajiwa kukamilika tarehe 6 mwezi ujao (Novemba, 2012).

“Katika awamu hii inayoendelea na awamu zijazo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea kukutana na makundi yote ya kijamii yaliyopo katika maeneo ambapo Tume inafanya mikutano yake,” amesema Katibu huyo wa Tume katika taarifa yake.

'Toa Maoni, Tupate Katiba'

No comments: