Tangazo

January 28, 2013

Lowassa anusurika katika ajali

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI MKUU aliyejiuzulu, Edward Lowassa, amenusurika katika ajali iliyotokea juzi katika eneo la Bwawani, mkoani Morogoro.

Mashuhuda wa tukio hilo, walisema kuwa gari la Lowassa lenye namba za usajili T 676 AWW, nusura likutane uso kwa uso na basi la Kampuni ya Moro Best na badala yake liligongwa ubavuni.

Kwa mujibu wa mashuhuda hao, chanzo cha ajali hiyo kilitokana na mabasi mawili yaliyokuwa yakifukuzana, likiwemo basi la Moro Best.

Ilielezwa kuwa, mabasi hayo yalipofika eneo la Bwawani, dereva wa Moro Best alitanua njia kutaka kulipita basi walilokuwa wakifukuzana nalo, ghafla alijikuta akikalibiana uso kwa uso na gari la Lowassa lililokuwa likitokea jijini Dar es Salaam.

“Dereva wa gari la Lowassa alipoona anakutana uso kwa uso na basi la Moro Best, kwa ujasiri mkubwa aliamua kuliingiza gari hilo katikati ya magari mengine na katika kufanya hivyo, akajikutana gari lake likigongwa ubavuni,” alisema shuhuda wa tukio hilo.

Lowassa ambaye muda wote alikuwa amepigwa na butwaa, alipoulizwa kama amepata majereha alisema hakuwa na jeraha lolote.

Hata hivyo, alisema mkono wa Mungu ni mkubwa kwani alishuhudia jinsi gari lake na basi la Moro Best yalivyotaka kugongana uso kwa uso na hajui nini kimenusuru.

“Nililiona basi la Moro likitukabili uso kwa uso na gari langu na wakati hali hiyo inataka kutokea, nikakumbuka maneno ya wimbo mmoja hivi yanayosema “Hivi vyote vinatoka wapi? Hii ni huruma tu”.

Pamoja na ajali hiyo, Lowassa aliendelea na safari yake. Alikuwa akitoka jijini Dar es Salaam kwenda mkoani Morogoro kwenye harambee ya kanisa moja mjini humo.

No comments: