Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk.Charles Kimei (kushoto) akiongozana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu na Balozi wa China hapa nchini, Lü Youqing wakati wa hafla ya uzinduzi wa CRDB China Desk.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk.Charles
Kimei akitoa hotuba yake wakati wa uzinduzi wa CRDB China Desk
Balozi wa China hapa nchini, Lü Youqing akizungumza wakati wa uzinduzi wa CRDB Chine Desk.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu akizungumza katika hafla hiyo.
Baadhi ya wageni waalikwa.
DAR ES SALAAM, Tanzania
MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk.Charles Kimei,
amewataka wajasiriamali na wawekezaji wanaofanya biashara zao kati ya Tanzania
na China, kuchangamkia fursa pana ya ukuzaji mitaji yao na pato kwa kutumia
huduma mpya ya CRDB China Desk.
Dk Kimei aliyasema hayo jana wakati wa hafla ya uzinduzi wa
China Desk, inayotolewa na CRDB, itakayo wahudumia wafanyabiashara,
wajasiriamali na wawekezaji wanaofanyakazi zao baina ya mataifa hayo rafiki.
“China Desk, ni huduma yenye fursa inayoweza sio tu kusaidia
kukuza mitaji na kutanua wigo wa maendeleo, bali kudumisha ushirikiano wa
kiuchumi na maendeleo baina ya China na Tanzania, ambao uliasisiwa karibia nusu
karne iliyopita,” alisema Dk Kimei katika hafla hiyo.
Aidha, akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye
Hoteli ya Serena jijini, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na
Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, aliiomba CRDB kuboresha utoaji wa mikopo ya riba
nafuu kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, ili kuharakisha ukuaji wa pato la
Mtanzania na Taifa kwa ujumla.
Dk Nagu alibainisha kuwa, taasisi za kipesa nchini zina
mchango mkubwa kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kukuza pato lao,
kama zitakuwa tayari kuwapa mikopo yenye masharti nafuu na riba ndogo, ili
kusaidia harakati zao za kujikwamua na kukuza uchumi wa taifa.
“CRDB mnastahili pongezi kwa huduma hii, inayokuja wakati
ambao Tanzania kama Taifa, lilimpokea rais mpya wa China, Xi Jinping katika
ziara ya kikazi. Taasisi nyingine za kifedha zitambue umuhimu wa ushirikiano
baina ya mataifa haya na kubuni huduma kama hizi,” alisema Dk Nagu.
Aliongeza kwamba, kwa kuwa harakati za kumkomboa Mtanzania
zimeshika kasi, huku China ikijitoa kadri iwezavyo kuisaidia Tanzania, kuna
haja huduma kama hizo za China Desk zikaambatana na mikakati endelevu ya
kimandeleo, na taasisi nyingine nazo zinastahili kuiga.
Kwa upande wake, Balozi wa China hapa nchini, Lü Youqing,
aliipongeza CRDB kwa kufuata nyayo za waasisi wa China na Tanzania, kiasi cha
kubuni na kuzindua China Desk – dawati litakalowanufaisha wajasiriamali na
wafanyabiara wa kila upande.
“Huduma hii ni harakati chanya inayofuata nyayo za waasisi
wa ushirikiano baina ya China, Rais Mao Tse Tung na Tanzania, Mwalimu Julius
Nyerere. Vizazi na vizazi vitabaki kujivunia na kila mmoja atajisikia yu
nyumbani anapokuwa katika moja ya nchi hizo,” alisisitiza Youqing.
1 comment:
nice blog and article, thanks
Post a Comment