Tangazo

July 31, 2013

Mama Kikwete: Ndoa za utotoni ni moja ya sababu zinazowafanya watoto wa kike kukatisha masomo yao

Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda- Gaborone,  Botswana

Imeelezwa kwamba ndoa za utotoni ni moja ya sababu inayowafanya watoto wa kike kukatiza masomo yao huku asilimia 24 ya watoto hao  wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 18 wakiolewa katika nchi zilizopo kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Kutokana na umri wao watoto hao walitakiwa kuwa wanafunzi wa shule za Sekondari na siyo kuishi na wanaume hivyo basi jitihada za pamoja zinatakiwa ili kuhakikisha kuwa sheria na sera za kumlinda  mtoto wa kike na kumjengea mazingira salama ya kuishi zinatungwa.

Hayo yamesemwa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wajumbe waliohudhulia mkutano wa kamati maalum ya viongozi wanaoshughulikia huduma na elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) na Jumuia ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kikanda kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika katika Hoteli ya Lansmore Masa Square iliyopo mjini Gabarone nchini Botswana.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa mkutano huo unafanyika kipindi ambacho jitihada kubwa zinafanywa na nchi wanachama wa EAC na SADC ili kuhakikisha kuwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na mimba za utotoni zinapungua.

“Taarifa ya Kanda inaonyesha kuwa Ugonjwa wa Ukimwi ni changamoto kwa vijana wetu kwani  kati ya maaambukizi mapya 620,000 yanatokea kila mwaka  kuna  vijana wadogo wenye umri wa miaka 15hadi 24 kati ya hao asilimia  60% ni wasichana hii inamaana kuwa kwa  saa moja wasichana 31 na wavulana 21 wanapata maambukizi”, alisema Mama Kikwete

Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo jamii inatakiwa kuhakikisha kuwa kuwa mtoto wa kike anapata elimu  ingawa idadi ya watoto wa kike ni kubwa katika elimu ya msingi lakini wakifika elimu ya sekondari  idadi yao inapungua.

Mama Kikwete alisema, “Ingawa kuna jamii zingine ni mwiko kwa wazazi kuongea na watoto wao kuhusu afya ya uzazi lakini watoto hawa wanatakiwa kufahamu afya ya uzazi na mabadiliko ya miili yao  ili waweze kujikinga na ugonjwa wa Ukimwi na mimba za utotoni”.

Alisema nchini Tanzania kupitia Taasisi ya WAMA kuna kampeni isemayo mtoto wa mwenzio ni wako mkinge dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi ambayo inaihamasisha jamii kuwalinda watoto pia taasisi hiyo inafadhili  elimu ya sekondari kwa watoto ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.

WAMA imejenga mabweni ya wasichana katika shule za Sekondari, kutoa vifaa vya maabara,huduma ya maji safi na  kuhamasisha watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi pia kupitia klabu mbalimbali za wanafunzi mashuleni wametoa  elimu ya uzazi na jinsia ili vijana waweze  kujilinda na maambukizi ya HIV na kujikinga na mimba za utotoni.

Akifungua mkutano huo Prof. Alaphia Wright  kutoka UNESCO alisema mambo watakayoyajadili  yatapelekwa katika Serikali za nchi husika ili ziweze kuongeza msukumo wa kisera na kibajeti na  kuhakikisha kuwa wanatatua changamoto za afya na uzazi zinazowahusu vijana.

“Kama mnavyofahamu nchi zetu za kanda ya  Mashariki  na Kusini mwa Afrika zinakabiliwa na tatizo la idadi kubwa ya maambukizi mapya ya VVU kwa vijana hivyo basi elimu ya afya ya uzazi inatakiwa kutolewa  kwao  ambayo itawasaidia kupambana na ugonjwa huu pia wanahitajika  kupata taarifa sahihi ambazo zitawasaidi kuchagua nini cha kufanya kutokana na jinsia zao na matarajio yao ya baadaye”, alisema Prof. Wright.

Kwa upande wake Msaidizi wa waziri wa Afya wa Botswana Gaotlhaetse Matlhabaphiri alisema katika kipindi cha miaka 30 nchi nyingi Duniani zimekuwa zikipambana na ugonjwa wa Ukimwi na kuweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani hivi sasa jamii inaelewa jinsi ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Tunakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na idadi kubwa  ya watu ambayo haiendani na huduma zinazotolewa za kuzuia maambukizi ya HIV, ukosefu wa upatikanaji wa huduma za afya, hali mbaya ya uchumi ambao inaongeza kasi ya maambukizi ya ugnjwa huo hasa kwa vijana”, Matlhabaphiri.

Mkutano huo wa siku mbili umeandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupamba na Ukimwi (UNAIDS) , UNFPA, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF), Shirika la Chakula Duniani (WHO), UNESCO lengo kuu likiwa ni  kuhakikisha kuwa vijana wote wanapata elimu kuhusiana na afya ya uzazi na ujinsia jambo ambalo litawasaidia waweze kufahamu zaidi  ugonjwa Ukimwi.

No comments: