Tangazo

October 15, 2013

CRDB BENKI YASHIRIKI MAONESHO YA SEKTA YA NYUMBA


DAR ES SALAAM, Tanzania

WAZIRI wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, ameitaka Benki ya CRDB kuongeza kasi ya kuielimisha jamii kutumia fursa zitokanazo na huduma yake ya Jijenge, ili kusaidia harakati chanya za Serikali kuboresha maisha ya Watanzania.

Profesa Mbarawa alitoa wito huo, alipotembelea banda la CRDB katika uzinduzi wa Maonesho ya Tatu ya Sekta ya Nyumba nchini (Tanzania Homes Expo 2013), yanayofanyika kwa siku mbili kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

“Maisha bora kwa kila Mtanzania yanajumuisha pia makazi bora kwa wananchi, hivyo CRDB inapaswa kuwafikia wafanyakazi na wasio wafanyakazi, maofisini na majumbani, ili kutoa elimu ya kutosha ya mikopo hii ya Jijenge,” alisema Profesa Mbarawa.

Aliongeza kuwa, Watanzania wengi majumbani hawajafikiwa na elimu ya upatikanaji wa mikopo nafuu ya nyumba na pesa za kujengea, hivyo Huduma ya Jijenge ina nafasi kubwa ya kuisaidia Serikali katika kuwapatia wananchi makazi bora na ya kisasa.

Kwa upande wake, Meneja wa Mikopo ya Nyumba wa CRDB (Mortgage Business Unit), Silas Katemi, alisema benki yake inaupokea ushauri huo wa serikali na tayari ilishaanza kuufanyia kazi kwa kuzitembelea zaidi ya taasisi 40 kutoa elimu hiyo kwa wafanyakazi.

“Jijenge ni huduma mpya na CRDB imefanya harakati za kutoa na kufikisha elimu kwa wateja na wasio wateja. Tunaahidi kuendelea kutumia fursa tulizonazo katika kutoa elimu zaidi na kufikia mwisho wa mwaka huu tutakuwa tumeitangaza zaidi,” alisema Katemi.

Alifafanua kwamba, Huduma ya Jijenge inamuwezesha mkopaji kupata pesa ama nyumba na kulipia hadi kipindi cha miaka 20, ingawa kuna uhuru wa kuamua kwa mteja kulipa katika kipindi kifupi kutokana na pato lake, huku mkopo wake ukiwa na bima.

Aidha, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya EA Group inayoratibu maonesho hayo, Imani Kajula alisema kuwa Tanzania Homes Expo ni jukwaa huru linalowakutanisha wazalishaji na watoaji wa huduma katika Sekta ya Makazi na wateja wao.

Alibainisha kuwa, EAGroup wanajivunia ongezeko kubwa la kampuni shiriki katika maonesho hayo, kutoka 25 katika mwaka wa kwanza (2011), hadi kufikia kampuni 70 mwaka huu, inalothibitisha ubora wa maonesho na tija zake katika uzalishaji.
Meneja Mikopo ya Nyumba wa benki ya CRDB, Silas Katemi (katikati) akimuelezea Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa (kushoto), kuhusu mikopo nafuu ya nyumba inayotolewa na benki hiyo wakati wa Maonesho ya Sekta ya Nyumba “Tanzania Homes Expo” yaliyoanza jijini Dar es Salaam.
 Ofisa Masoko wa Benki ya CRDB, Julius Ritte akimuonesha jarida lenye maelezo ya kuhusu mikopo ya nyumba. Katikati ni Ofisa Mikopo wa benki hiyo, Aziza Mohamed
Baadhi ya wateja wa CRDB wakipata maelezo katika walipotebelea banda la benki hiyo.
Maofisa wa benki ya CRDB wakiwa katika picha ya pamoja.

No comments: