Na Zitto Kabwe
Napenda kuujulisha umma kwamba leo Ijumaa tarehe 4 Oktoba,
2013 nimewasilisha kwa Katibu wa Bunge muswada binafsi Bungeni kufuta Sheria ya
Magazeti ya mwaka 1976.
Changamoto iliyopo ni Sheria mbadala ya vyombo vya habari
baada ya Sheria ya sasa kufutwa. Hata hivyo wadau wa habari kama Baraza la
Habari Tanzania wameshafanyia kazi suala hili kwa muda mrefu sana na wana
mawazo kuhusu sheria mbadala.
Nimejulishwa kuwa muswada wa sheria mpya ya
habari tayari upo. Kwa hiyo katika mchakato wa kujadili muswada binafsi wa
kufuta sheria ya magazeti ya mwaka 1976 mabadiliko yanaweza kufanywa ili
kutunga sheria mpya. Hatua ya kwanza ni kuifuta sheria hii kandamizi ambayo
kiukweli tumechukua muda mrefu sana na baada ya madhara makubwa kufikia hatua
ya muswada wa kuifuta.
Nimeamua kutumia njia za kawaida za kuwasilisha muswada na
kuepuka njia ya dharura ili kujenga mazingira ya wadau wa habari kushiriki vya
kutosha katika mabadiliko yanayotakiwa. Njia ya dharura ni ya haraka lakini
huziba fursa za kupata maoni ya wadau ambao kimsingi ndio wenye sheria yenyewe
haswa. Hivyo nimepeleka muswada leo ili uchapwe kwenye gazeti la Serikali (GN)
kwa mujibu wa kanuni za Bunge, kisha usomwe kwa mara ya kwanza, uende kwa wadau
kwa mjadala na marekebisho na kisha kusomwa kwa mara ya pili na kupitishwa na
Bunge.
Ikumbukwe kuwa juhudi za kufuta sheria hii ni juhudi za
wadau wa tasnia ya habari na ni juhudi walizofanya kwa muda mrefu sana. Mimi
kama Mbunge ninawasilisha tu kwa sababu taratibu zetu za kuandika sheria
zinataka ama Serikali, Kamati ya Bunge au Mbunge kuwasilisha muswada. Kwa muda
mrefu tumewaangusha wana habari kwa kutosukuma vya kutosha mabadiliko
waliyokuwa wanayapigania. Hata hivyo, kuna msemo wa kihindi 'asubuhi huanza
pale unapoamka'. Sasa tuchukue hatua za kufuta sheria hii kandamizi.
Zitto Kabwe,Mb
Kigoma Kaskazini
No comments:
Post a Comment