Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko
wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Crescentius Magori, akifafanua
jambo mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa tano wa wadau wa NSSF, uliofanyika
mwishoni mwa wiki jijini Mwanza. (Picha na Sitta Tuma)
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Ndikilo (wa tatu kushoto), Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Crescentius Magori (wa pili kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Mkutano Mkuu jijini Mwanza.
Na Sitta Tumma, Mwanza
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umetenga zaidi ya sh. Bilioni 72.8 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa hoteli ya kitalii, itakayokuwa na nyota tano katika jiji la Mwanza.
Mbali na mradi huo, NSSF pia imekusudia kuanza ujenzi wa nyumba 500 kwa ajili ya kuuza kwa wananchi na wanachama wa mfuko huo, ikiwa ni lengo la kuinua uchumi wa jamii na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi wa Utekelezaji wa NSSF, Crejcentius Magori, wakati alipozungumza kwenye mkutano mkuu wa tano wa wadau wa NSSF, uliofanyika ukumbi wa JB Belmont hoteli jijini Mwanza, uliowashirikisha maofisa wa migodi ya madini nchini.
Alisema kwamba, mkakati wa Mfuko huo wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii ni kuona jamii, wanachama wake na taifa zima wananufaika na kazi zake, na kwamba tayari mradi wa kitegauchumi hicho cha hoteli mkandarasi wake yupo eneo la mradi.
"NSSF imedhamiria kuwekeza zaidi katika miradi mingi ya kiuchumi hapa Mwanza, Kanda ya Ziwa na maeneo mengine nchini.
"Kwa sasa tumetenga bilioni 72.8 kwa ajili ya kujenga hoteli ya nyota tano hapo Capri-Point jijini Mwanza. NSSF pia tuna mpango wa kujenga nyumba 500 za wanachama wetu na jamii," alisema Mkurugenzi Magori.
Kwa upande wake, Meneja Mipango na Uwekezaji wa NSSF, Mseli Abdallah alieleza kwamba, mradi wa ujenzi wa nyumba upo katika hatua ya michoro, na kwamba ujenzi wa hoteli hiyo ya nyota tano utasaidia sana kukuza uchumi wa jiji la Mwanza.
Kwa mujibu wa Abdallah, NSSF imedhamiria pia kuwekeza miradi mbali mbali ya kiuchumi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, na kwamba kwa sasa kuna mradi wa jengo la kitega uchumi linajenga mjini Shinyanga.
Naye Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Ndikilo (RC), ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, aliwataka waajiri wote kulipa michango ya wafanyakazi wao katika mifuko ya jamii.
Alisema kwamba, kuna baadhi ya waajiri wamekuwa wakishindwa kutekeleza wajibu huo wa kulipa michango hiyo, na kutoa onyo kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaoshindwa kutekeleza suala hilo.
Aidha, aliupongeza uongozi wa Mfuko huo wa Taifa wa Hifadhi ya Jami kwa mikakati yake ya uwekezaji nchini, kwani kazi hiyo inachangia maradufu kuimarika kwa uchumi wa jamii na taifa zima.
No comments:
Post a Comment