Hiki ni moja ya kisima
cha gesi kilichopo Mnazi Bay eneo la nchi kavu kinachofikisha idadi ya visima
vitatu ambapo kimoja kipo eneo la bahari kuu.
|
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Eleuteri
Mangi-MAELEZO Mtwara
RASILIMALI za gesi
asilia, mafuta na madini zilizopo mikoa ya Lindi na Mtwara ni kwa neema,
ukarimu, ufadhili na baraka za Mwenyezi Mungu alizoipatia Tanzania zitumike kwa
manufaa ya wanachi wote.
Kauli hiyo ilitolewa na
Mgeni rasmi Askofu Mkuu wa kanisa la Anglikani Tanzania Dkt. Jacob Chimeledya
alipokuwa akifungua kongamano la Viongozi wa Dini leo katika ukumbi wa Chuo cha
Ufundi Stadi (VETA) mjini Mtwara.
Kongamano hilo la
viongozi wa dini liliongozwa na kauli mbiu iliyosema “Rasilimali zetu za gesi
asilia, mafuta na madini kwa amani na maendeleo ya Tanzania”.
Lengo la kongamano la
voingozi wa dini lilikuwa ni kupata elimu juu ya rasilimali hizo muhimu kwa
maendeleo ya kiuchumi kwa minajili ya haki, upendo na amani kwa kuzingatia sera
na taratibu za Serikali kwa maslahi ya wananchi wote.
“Pamoja na sheria na sera
za rasilimali za gesi, mafuta na madini zilizopo nchini, ni lazima ziongozwe na
misingi muhimu ya taifa letu” alisema Askofu Dkt.Chimeledya.
Dkt. Chimeledya
aliitaja misingi hiyo kuwa ni pamoja na haki ya kila mtanzania, ukweli juu ya
sera mipango na mikakati bora, mshikamano wa jamii, kujali maslahi ya wote na
ushirikishwaji wa jamii zilizo katika maeneo yanayozunguka sehemu zilipo
rasilimali mbalimbali nchini.
Kwa upande wake Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi alisema kuwa Serikali kupitia
Wizara yake ipo tayari kuendelea kushirikiana na vingozi wa dini wa wanachi
wote ili kuendelea kusukuma mbele maendeleo ya nchi kwa manufaa ya watu wake.
“Gesi ni ukombozi ni
ukombozi na itatusogeza mbele ambapo italinufaisha taifa katika Nyanja
mbalimbali, viwandani, majumbani na ndani ya nchi hata nje ya nchi” alisema
Maswi
Kugunduliwa kwa gesi
mikoa ya Lindi na Mtwara kumefungua milango ya kujengwa viwanda mabalimbali
ambavyo vinatajiwa punguza tatizo la ajira katika mikoa hiyo na nchi nzima kwa
ujumla.
Miongoni mwa viwanda
vya saruji vinavyoendelea kujengwa ni Dangote kilichopo Mtwara na Meis
kilichopo mkoani Lindi.
Katibu Mkuu Maswi
ametoa rai kwa watanzania wenye uwezo wa kuwekeza kupitia viwanda wafikirie
kuwekeza juu ya viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumia malighafi
zinazotokana na mabaki gesi baada ya kuchakatwana ikiwemo viwanda vya mbolea,
plastiki, chupa na nguo.
Viongozi hao wa dini
walipata fursa ya ziara ya kutembelea mitambo ya kusafisha gesi na visima vya
gesi Mnazi Bay eneo la Msimbati na eneo la juenzi wa mitambo ya kusafisha na kuchakata
gesi kilichopo eneo la Madimba mkoani Mtwara.
Kongamano kwa viongozi
wa dini ni la siku mbili ambapo linawashirikisha viongozi wa dini mbalimbali za
kikristo na kiislam kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara pamoja na viongozi na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya
Nishati na madini na mashirika yaliyo chini yake ya TANESC, TPDC NA REA.
Kongamano hilo ni muendelezo ulitokana na
kongamano kama hilo lililofanyika Januari 2014 jijini Dar es salaam ambapo
wajumbe kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara waliona kuna haja wao kama wadau wa
gesi, mafuta na madini wapate elimu kama hiyo kwa manufaa ya wanachi wa mikoa yao
na nchi nzima.
No comments:
Post a Comment