Waziri wa Katiba na Sheria Dk.
Asha-Rose Migiro akiwasilisha taarifa ya makadirio ya bajeti ya Wizara yake kwa
Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala jana (Jumamosi, Mei 3, 2014).
Kulia kwake ni Naibu wake Angellah Kairuki na wa pili kulia ni Mwenyekiti wa
Kamati hiyo Wiliam Ngeleja. Picha na Wizara ya Katiba na Sheria.
---------
Na Omega Ngole
Serikali imesisitiza nia yake ya kuendesha shughuli zake kwa
uwazi na kusema maandalizi ya kutunga sheria ya haki ya kupata taarifa kutoka
kwa taasisi za umma yameanza kuongeza uwazi katika uendeshaji wa shughuli za
serikali.
Akiwasilisha taarifa ya makadirio ya matumizi kwa mwaka ujao
wa fedha kwenye Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala jijini Dar es
Salaam jana (Jumamosi, Mei 3, 2014), Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose
Migiro alisema dhamira hiyo inatokana na matakwa ya Katiba kuhusu haki ya
kupata taarifa, Mpango wa Kimataifa wa Uendeshaji wa Serikali kwa Uwazi (OGP)
na ahadi ya Rais Kikwete.
“Azma ya Serikali ni kuendesha shughuli zake kwa uwazi zaidi
katika Nyanja mbalimbali za huduma…hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba
sambamba na Mpango wa Kimataifa wa Uendeshaji wa Serikali kwa Uwazi (OGP),”
alisema Waziri Migiro na kuongeza:
“Wizara imeandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu kutunga
sheria ya Haki ya Kupata Taarifa kutoka taasisi za umma na ni matarajio ya
Wizara kuwa mchakato huu utakamilika kabla ya mwezi Disemba, 2014,” alisema
katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria
Angellah Kairuki na viongozi wengine wa Wizara na taasisi zake.
Katika mkutano huo, Waziri Migiro pia alizungumzia mpango wa
Wizara yake wa kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani ambapo Mahakama ya
Tanzania imeanzisha mpango wa ufanyaji kazi kwa kujipima.
Kwa mujibu wa Dkt. Migiro, utaratibu huo unaweka wastani wa
idadi ya mashauri yatakayotolewa uamuzi na Majaji na Mahakimu katika kila ngazi
ya Mahakama kwa kila mwaka.
“Katika Mahakama ya Rufani lengo ni kumaliza wastani wa
mashauri 1,200 hadi 1,400 kwa mwaka, Mahakama Kuu mashauri 200 hadi 250 kwa
kila Jaji kwa mwaka , na Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya mashauri 250 hadi
300 kwa kila Hakimu kwa mwaka,” alisema Waziri Migiro katika mkutano huo
ulioongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja.
Waziri Migiro, ambaye aliteuliwa na Rais Kikwete kuongoza
Wizara hiyo mapema mwaka huu, alifafanua kuwa utaratibu huo umeshaanza kufanya
kazi na umeonyesha mafanikio makubwa.
Pamoja na utaratibu huo, Waziri Migiro pia alizungumzia
jitihada za Serikali za kupunguza mlundikano wa wafungwa na mahabusu magerezani
kupitia mpango maalum wa kutenganisha shughuli za mashtaka na upelelezi.
Kwa mujibu wa Waziri Migiro, kupitia mpango huu, Mkurugenzi
wa Mashataka huchuja majalada yanayowasilishwa kwake na taasisi za upelelezi
kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa.
“Mkurugenzi wa mashtaka ndiye mwenye mamlaka ya kutoa hati
ya mashtaka baada ya kujiridhisha na ushahidi unaowasilishwa na vyombo vya
upelelezi, hivyo kupunguza kwa mlundikano wa mashauri mahakamani kutokana na
utaratibu huu wa kuchuja majalada,” alisema na kuongeza:
“Idadi ya Mahabusu mageezani imepungua kutoka 18,203 mwezi
Juni, 2012 na kufikia 17,284 mwezi Machi, 2014 na idadi ya wafungwa imepungua
kutoka 17,548 mwezi Juni, 2013 na kufikia 16,547 mwezi Machi, 2014,”
alisema.
Wakizungumza baada ya Waziri Migiro kuwasilisha taarifa
yake, Wajumbe wa Kamati hiyo waliipongeza Serikali kwa mikakati iliyoanzisha ya
kuondokana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya sheria.
“Huu mpango wa Mahakama wa kujipima wenyewe sisi
tumefurahishwa nao sana,” alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, William Ngeleja
ambaye aliungwa mkono na mjumbe mwingine wa Kamati hiyo na Mbunge Wa Ngara,
Deogratius Ntukamazina.
Pamoja na pongezi hizo, wajumbe wa kamati hiyo waliitaka
serikali kuongeza jitihada za kuondokana na changamoto zinazoikabili Wizara
hiyo zikiwemo uhaba wa watumishi na ufinyu wa bajeti.
“Bajeti ya Wizara hii inayojumuisha mhimili wa Mahakama ni
ndogo sana,” alisema Nimrod Mkono, mjumbe wa Kamati hiyo na Mbunge wa Musoma
Vijijini ambaye aliungwa mkono na Nyambari Nyangwine, Mbunge wa Tarime.
No comments:
Post a Comment