Tangazo

May 2, 2014

MKURUGENZI WA IDARA YA HABARI (MAELEZO) ATOA UFAFANUZI ‘TUZO YA JAJI WARIOBA’

Assah Mwambene

Na Magreth Kinabo,

Maelezo


Mkurugenzi  wa Idara  ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene amesema Jaji Joseph Warioba alitunukiwa tuzo ya muungano iliyotukuka   kwa kuwa alistahili kupewa kama viongozi wengine na  kuwa kitendo si kumkejeli kama baadhi ya vyombo vya habari vilivyoripoti  hivi karibuni.

 Hayo yalisemwa juzi na Mkurugenzi huyo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu  suala hilo katika  mkutano na waandishi wa habari uliofanyika  kwenye ukumbi wa  MAELEZO jijini Dares Salaam.

“Kumekuwa kuna taarifa katika baadhi ya magazeti kuwa Serikali kumpa tuzo Jaji Warioba ni kumkejeli, Ninapenda kuwataarifu kuwa  kitendo cha Serikali kumpa tuzo Jaji Warioba haikumkejeli wala kumtukana. Jaji Warioba anastahili kupewa tuzo kama mawaziri wakuu wengine kwa kuwa mchango wake katika  muungano unajulikana,” alisema Mwambene. 

Tuzo hiyo aliyoipewa Jaji Warioba, wakati wa maadhimisho ya mika 50 ya Muungano wa Tangayika na Zanzibar.

 Mwambene aliongeza kuwa  tuzo hiyo haihusiani na mjadala wa  Rasimu ya Katiba.

 Alifafanua kuwa katika mjadala wa Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba uliokuwa ukifanyika katika Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma, baadhi ya wajumbe walikuwa wanatoa mawazo yao na si kwamba wanapingana na Jaji Warioba 

“ Mjumbe anatoa mawazo yake wakati wa kujadili  kwa kuwa hiyo bado ni rasimu, hivyo  hapingani  na Jaji Warioba,” alisisitiza huku akisema rasimu huwa inafanyiwa marekebisho.

Katika hatua nyingine,Mkurugenzi huyo , alisema bado Ofisi yake inaendelea na hatua ya pili kuhusu gazeti la MAWIO kutoa maelezo ya kuchapisha habari yenye kichwa cha habari ‘Hati  Muungano Utata’.

Mwambene alifafanua kuwa ofisi hiyo inaendelea na suala hilo kwa hatua hiyo ili kutoa nafasi kwa viongozi husika wa gazeti  kutoa maelezo baada ya hapo awali  kupeleka  barua ya kutaka maelezo hayo kwenye Ofisi za  gazeti la ‘MAWIO’ na kukuta zimefungwa.

 Aidha alisema kuwa hata majirani wa ofisi hizo walikataa kupokea barua hiyo, kwa maelezo kuwa kama ni masuala  ya habari  wahusika ndio wanapaswa kuipokea.

Aliongeza kwamba ofisi yake itafanya maamuzi sahihi ikiwahaitapata maelezo hayo, hivyo isijeikalaumiwa.

Mwambene aliwataka waandishi wa habari kuwa na kitambulisho  cha  uandishi wa habari (Press Card) na ametoa muda wa wiki moja kuanzia leo kwa mwandishi ambaye hana ili kuweza kukamilisha taratibu za kukipata.

Pia amewataka waandishi wa habari kuwa na heshima  katika utendaji kazi wa taaluma hiyo na kuzingatia mavazi yanayostahili kwani wao ni kioo cha jamii.

No comments: