Baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya
Katiba na Sheria katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo
uliofanyika jijini Dar es Salaam Jumatano, Aprili 30, 2014.
XXXXXXXXXXXXXXX
Na Martha Komba,
Dar es Salaam
Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wametakiwa kufanya
kazi kwa bidii ili kuongeza ufanisi katika utendaji wao.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Fanuel Mbonde
amesema hayo katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo uliofanyika
leo (Alhamisi April 30, 2014) jijini Dar-es-salaam.
“Uwajibikaji ni suala muhimu sana katika utumishi wa umma,”
alisema katika mkutano huo wa siku moja uliofanyika katika ukumbi wa Wizara
hiyo jijini Dar-es-salaam.
Aidha, Katibu Mkuu huyo aliwasihi watumishi wote wa Wizara
yake kuungana na wafanyakazi wote nchini na duniani kushiriki katika sherehe za
Siku ya Wafanyakazi zinazofanyika kesho (Alhamisi, Mei 1, 2014).
Awali akiongea katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha
Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Mkoa wa Dar-es-salaam Bw. Hassan Kaumo
aliwataka watumishi wa Wizara hiyo kutimiza wajibu wao katika sehemu zao za
kazi.
“Tunapodai maslahi ni lazima pia tusisitize kutimiza wajibu.
Wafikishieni salamu hizi wafanyakazi wote, wachape kazi ili watupe viongozi
nguvu ya kudai maslahi bora,” alisema Kaumo katika mkutano huo uliohudhuriwa na
viongozi na wawakilishi wa wafanyakazi kutoka Idara na Vitengo vyote vya Wizara
hiyo.
Mkutano huo, pamoja na mambo mengine, ulijadili maslahi ya
watumishi na kupitia na kuridhia Taarifa ya Mpango wa Bajeti ya Wizara hiyo kwa
mwaka ujao wa fedha 2014/2015.
No comments:
Post a Comment