Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Uongozi wa Shirika la NEC
Corporation la Japan, wakiongozwa na Rais wao Dkt. Nobuhiro Endo, wakati
walipofika ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Septemba 12, 2014 kwa
ajili ya mazungumzo. Picha na OMR
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Mheshimiwa Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo amekutana na Uongozi
wa Kampuni ya NEC yenye makao yake makuu jijini Tokyo nchini Japan. Ujumbe wa
NEC-Japan umeongozwa na Rais wa Kampuni hiyo inayojishughulisha na masuala ya
Mawasiliano na Teknolojia, Dkt. Nobuhiro Endo.
Ujio wa Kampuni hii nchini Tanzania unatokana
na mwaliko wa Tanzania kwa makampuni ya Japan kufuatia ziara ya kikazi
aliyoifanya Mheshimiwa Makamu wa Rais nchini Japan, mwezi wa Mei mwaka huu.
Mheshimiwa Makamu wa Rais alitembelea Makao Makuu ya Kampuni hiyo wakati za
ziara hiyo.
Katika mazungumzo na uongozi wa NEC Mheshimiwa
Makamu wa Rais aliwaeleza wageni wake nia ya Tanzania kuona inatanua
mawasiliano na teknolojia nchini ili kuinua uchumi na akafafanua kuwa
teknolojia yoyote kutoka NEC inakaribishwa hapa nchini ili kusaidia Tanzania
kupiga hatua.
Uongozi wa NEC nao ulimueleza Mheshimiwa
Makamu wa Rais kuwa, NEC inaushirikiano wa karibu na Shirika la Simu Tanzania
(TTCL) na kwamba wanatarajia kukutana na uongozi wa wizara ya Mambo ya Ndani
kwa lengo la kutazama fursa za kusaidia teknolojia katika ulinzi.
Imetolewa na:
Ofisi ya Makamu wa Rais
Ikulu Dar es Salaam
Septemba 12, 2014
No comments:
Post a Comment