Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Angellah Kairuki (MB) akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya
Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza Jaji Kiongozi Mstaafu Hamis Amir Msumi (kushoto) na
Wajumbe wengine wa Tume hiyo, Majaji Wastaafu Stephen Ihema (kulia) na Vincent
Lyimo ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo (Oktoba 22, 2014)
xxxxxxxxxxxxxxxx
Na
Mwandishi wetu
Serikali imeahidi
kuendelea kuiwezesha na kuipa ushirikiano Tume ya Rais ya Uchunguzi wa
Operesheni Tokomeza ili iendelee kutekeleza na hatimaye kukamilisha majukumu
yake kama ilivyokusudiwa.
Naibu Waziri wa Katiba
na Sheria Mheshimiwa Angellah Jasmine Kairuki amesema hayo jijini Dar es Salaam
leo (Jumatano, Oktoba 22, 2014) wakati akizungumza na Wajumbe wa Tume hiyo
waliomtembelea ofisini kwake ili kubadilishana mawazo.
“Serikali itaendelea
kuwapa ushirikiano na kuwawezesha ili mtekeleze majukumu yenu kama
ilivyokusudiwa,” amesema Naibu Waziri katika mkutano huo uliohudhuriwa na
Mwenyekiti wa Tume Jaji Kiongozi Mstaafu Hamis Amir Msumi na Wajumbe wengine
Jaji Mstaafu Stephen Ihema, Jaji Mstaafu Vincent Lyimo na Katibu wa Tume hiyo
Wakili Fredrick Manyanda.
Ahadi ya Naibu Waziri
Kairuki ilifuatia kauli ya Mwenyekiti wa Tume hiyo kuwa Tume yake imekuwa
ikipata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi na Serikali tangu
ilipoteuliwa tarehe 1 Mei mwaka huu.
“Tunashukuru kwa
ushirikiano tunaoupata kutoka Serikalini,” amesema Jaji Msumi na kufafanua
kuwa viongozi wa Serikali wa wilaya na mikoa wametoa ushirikiano mzuri kwa Tume
yake katika awamu ya kwanza ya kukusanya taarifa na malalamiko.
Jaji Msumi amesema
kuwa katika awamu hiyo iliyofanyika katika mikoa ya Kigoma, Katavi,
Rukwa na Mbeya wananchi na viongozi wa Serikali katika maeneo hayo
walitoa ushirikiano mkubwa.
“Wakuu wa Wilaya na
Wakurugenzi wa Halamashauri walitupa ushirikiano wa kutosha na wananchi
walikuwa na shauku kubwa ya kukutana na Tume,” amesema Jaji Msumi alipokuwa
akizungumzia awamu ya kwanza ya ziara ya Tume yake iliyofanyika kuanzia tarehe
17 Septemba, 2014 hadi 6 Oktoba mwaka huu.
Jaji Msumi pia
amemweleza Naibu Waziri kuwa Tume yake inatarajia kuanza awamu ya pili ya
kutembelea mikoa sita ya Kanda ya Ziwa kuanzia kesho (Alhamisi, Oktoba 23,
2014) hadi tarehe 18 Novemba mwaka huu ili kukusanya taarifa na malalamiko
katika kuhusu Operesheni Tokomeza. Mikoa itakayotemebelea na Tume hiyo ni
Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara.
Rais Jakaya Kikwete, kwa mujibu wa Kifungu cha 3 cha
Sheria ya Uchunguzi Sura ya 32, aliunda Tume ya Uchunguzi (Commission of Inquiry) kuhusu vitendo
vilivyotokana na uendeshaji wa Operesheni Tokomeza tarehe 1 Mei mwaka huu.
No comments:
Post a Comment