Tangazo

November 18, 2014

Mfanyabiashara maarufu Bw. Macha ana kesi ya kujibu yasema Mahakama ya Kisutu

Na Mwandishi Wetu

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imetoa uamuzi katika kesi inayomkabili mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam, Hans Aingaya Macha (pichani) kuwa ana kesi ya kujibu.

Uamuzi huo, umetolewa na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Devotha Kisoka jana katika kesi inayomkabili mfanyabiashara huyo ya kugushi hati ya kiwanja cha Ramadhan Balenga chenye namba 183 kilichopo Kigogo, mkataba wa mauziano na hati ya uhamishaji miliki.

Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Devotha alisema baada ya kupitia ushahidi wa awali wa upande wa mashitaka, mshitakiwa(Macha) una kesi ya kujibu na mahakama inakutaka uanze utetezi katika kesi yako inayokukabili na dhamana yako inaendelea kama kawaida.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Devotha aliiharisha kesi hiyo hadi Desemba Mosi kwa upande wa mshitakiwa kuanza kutoa ushahidi wake, mahakamani hapo katika kesi hiyo inayoonekana kuvuta hisia kubwa za wananchi jijini Dar es Salaam.

Kabla ya mahakama kutoa uamuzi huo, Wiki iliyopia Hakimu Devotha alisikiliza ushahidi wa mwisho kutoka kwa upande wa mashitaka, ambaye alikuwa Mkuu wa Maabara ya Uchunguzi wa Hati wa Polisi, Mrakibu wa Polisi, Amaan Renatus Saad.

Renatus alidai mahakamani hapo, mbele ya Hakimu Devotha kuwa alipokea nyaraka kutoka kwa Ofisi ya Msajili wa Hati ikiomba ifanyiwe uchunguzi katika nyaraka za uhamishaji miliki kutoka kwa Balenga kwenda kwa Macha.

"Nina uzoefu wa miaka zaidi 10, ambapo nimeupata sehemu mbalimbali ikiwemo Bostwana. Polisi ilipokea barua kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutaka kufanyiwa uchunguzi,''alidai.

Renatus alidai baada ya kupokea barua, walifanya uchunguzi na kutoa taarifa kwa Wizara ya Ardhi kuwa saini walizochunguza hazikusaini na mtu mmoja, ambaye ni Balenga, hivyo zimegushiwa.

Alidai uchunguzi wao, ulizingatia mambo mengi ikiwemo mgandamizo wa peni, spidi ya peni, hivyo aliiomba mahakama ipokee ushahidi wake kama kielelezo sahihi katika kesi hiyo na upande wa mashitaka unaoongozwa na Wakili wa serikali, Nassoro Katuga, alidai mahakamani hapo kuwa, wamefunga ushahidi na kutoa nafasi ya upande wa utetezi nao kutoa ushahidi wake.

No comments: