Tangazo

July 9, 2015

JAMII YATAKIWA KUSHIRIKI KUPUNGUZA AJALI ZA BARABARANI

Na Magreth Kinabo

Imeelezwa kwamba ajali za barabarani yanasababisha  vifo vya watu milioni 1.24 kila mwaka duniani.

Aidha watu kati ya 20 milioni na 50 milioni huumia kutokana na ajali za barabarani.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Idara ya  Uhakiki  wa Huduma Bora za Afya Dk. Mohamed Ali Mohamed  kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO)ya mwaka 2013 ,wakati wa semina ya waandishi wa  habari kuhusu usalama barabarani iliyofanyika jijini Dares Salaam.

Semina ambayo inaambatana na wiki ya Umoja wa Mataifa ya Usalama Barabarani ambayo imeanza Julai 9 na kilele chake Julai 15 katika Shule ya Msingi ya Uhuru Mchanganyiko iliyopo jijii humo, ambapo mwaka huu imelenga kupunguza ajali za barabarani kwa watoto. 

Aliongeza kwamba  asilimia kubwa (90%) ya vifo vya ajali za barabarani yanatokea katika nchi ambazo zina uchumi wa kati na wa chini.

Hali ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani kwa nchi ambazo ziko chini ya Jangwa la Sahara ni  (24.1 kwa kila vifo 100,000) ukilinganisha na idadi ya vifo  kwa dunia nzima (18 kwa kila vifo 100,000). Hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na hali mbaya ya barabara zetu.

Alisema taarifa ya polisi inaonyesha kuwa katika kipindi cha 2008 mpaka 2013 nchini Tanzania kumekuwa na magari yaliyosajiliwa ni 500,000 ongezeko hili linaenda sambamba na ongezeko la vifo vinavyotokana na ajali nchini, kutoka vifo 309 mwaka 2008 mpaka vifo 930 mwaka 2012.

Aidha Dk .Mohamed alisema ripoti ya Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) inaonyesha asilimia 95% ya ajali za barabarani zinasababishwa na matumizi mabaya ya barabara.

“Sekta ya Afya ina mchango mkubwa katika kukabiliana na majeruhi wa ajali, aidha wingi wa ajali na kupelekea majeruhi wengi ni changamoto katika sekta ya afya. Madhara yanayotokana na hizi ajali hupunguza maendeleo ya nchi.

“Hivyo ni muhimu sote kwa pamoja tuweke juhudi za dhati kupunguza ajali za barabarani,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Mary Kitambi kutoka Wizara hiyo alisema ajali za barabarani huigharimu Serikali sh. bilioni 3.4 kila mwaka kwa ajili ya matibabu ya watu waliojeruhiwa.

Mwakilishi kutoka WHO, ambaye ni Afisa Miradi, Mary Kessi  alisema  kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo ya mwaka 2010 watoto 186,300 hufariki kila mwaka  kwa ajali za barabarani.

Aliwataka waandishi wa habari  kuripoti kwa kufanya utafiti juu ya vyanzo vya ajli za barabarani badala ya madhara pekee. 

Kwa upande wake Mkaguzi wa Polisi Mossi Ndozero aliwataka jamii kujenga tabia ya kutii sheria bila shuruti ili kuweza kupunguza ajali ya barabarani na kutoa taarifa  za madereva wanaokiuka sheria za barabara  kwa kutumia namba za simu 0800 757575 na 0682 887722.

No comments: