Tangazo

October 9, 2015

BAKHRESA AIPIGA JEKI TASWA

Mwenyekiti wa Taswa, Juma Pinto
 
KAMPUNI ya Said Salim Bakhresa (SSB) Group Limited, imetoa kiasi cha Sh. Milioni 10 kwa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kwa ajili ya tuzo za Wanamichezo Bora nchini, zilizopangwa kufanyika Oktoba 12, mwaka huu.
 
Pia TASWA inatarajia kutoa Tuzo ya Heshima kwa Rais Jakaya Kikwete ikiwa ni kuthamini mchango wake katika michezo wakati wa uongozi wake.
 
TASWA imefarijika sana na udhamini huo wa SSB, hasa wakati huu ambapo chama hicho kipo katika maandalizi ya mwisho kuelekea katika tuzo hizo.
 
Licha ya kutoa kiasi hicho cha fedha,  pia SSB (Azam) itatoa ving’amuzi kwa wanamichezo wote 15 watakaopewa tuzo siku hiyo.
 
Tuzo hizo zitafanyika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, ambapo wachezaji 10 waliong’ara zaidi katika miaka 10 ya Rais Kikwete watapewa tuzo pamoja na viongozi watano wa michezo waliofanya vizuri pia watapewa tuzo.
 
Wadhamini wengine wa tuzo hiyo ni Kampuni ya GSM Foundation na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
 
Imetolewa na:
Juma Pinto
Mwenyekiti TASWA

No comments: