Tangazo

October 5, 2015

MAGUFULI AMSHAWISHI MO KUJENGA KIWANDA SINGIDA ILI KUTOA FURSA YA AJIRA

IMG_4556
Mgombea urais kupitia tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli akimwaga sifa kwa aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Singida Mjini (Mbunge Mstaafu), Mohamed Dewji baada ya kutumikia vyema na kwa uadilifu kiti chake cha Ubunge jimboni humo wakati wa mkutano wa kampeni za mgombea urais huyo kwa tiketi ya CCM uliofanyika katika viwanja wa Peoples mjini humo.

Na Nathaniel Limu, Singida

MGOMBEA urais kupitia CCM Dk.John Pombe Magufuli,amemshawishi aliyekuwa mbunge wa jimbo la Singida mjini Mohammed Dewji,kujenga kiwanda mkoani humo, ili pamoja na mambo mengine,kupunguza uhaba wa ajira.

Amedai Dewji maarufu kwa jina la MO katika kipindi chake cha ubunge miaka 10 iliyopita, ameonyesha mapenzi makubwa na ya aina yake kwa wakazi wa jimbo la Singida na mkoa kwa ujumla.

Dk.Magufuli alisema kutokana na ukweli huo,sasa anapaswa kuhamishia mapenzi hayo kwa kujenga kiwanda mkoani Singida kitakachoajiri vijana, na pia kuinua pato la mkoa na taifa kwa ujumla.

Mgombea urais huyo aliyasema hayo kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Peoples mjini Singida na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa jimbo la Singida na maeneo ya jirani.

“Katika kipindi chako cha ubunge umeonyesha uzalendo wa hali ya juu,umewatumikia vema wananchi wa jimbo la Singida mjini. Ndio maana hadi sasa bado wana mapenzi makubwa sana kwako,naomba uwajengee kiwanda. Nakuhakikishia mimi binafsi napenda wawekezaji wazalendo wanaoipenda nchi yao na wewe ni mmoja wao”,alisema Dk.Magufuli.

Aidha, Dk.Magufuli amemuahidi kumpa ushirikiano pindi atakapohitaji kuwekeza katika viwanda mkoani Singida.

Akisisitiza,alisema “Dewji nakuomba sasa sana ikiwezekana jenga hata viwanda vitatu ili wananchi wa mkoa wa Singida wapate ajira. Nitakuunga mkono kwa asilimia 100.Kama ni kibali unataka,nitakupa leo hii kwa kuwa mmenihakikishia nitakuwa rais wa tano”.

Awali akizungumza kwenye mkutano huo wa kampeni, Dewji aliwaahidi wakazi wa jimbo la Singida mjini kwamba ataendelea kushirikiana nao katika kulipaisha jimbo hilo kimaendeleo.
IMG_4554
“Mimi nimezaliwa hapa nyumbani kwetu Singida mjini na kitovu changu kimezikwa hapa hapa.Kutoka chini ya sakafu ya moyo wangu,niwahakikishie kwamba nalipenda sana jimbo letu hili la Singida mjini.Nitaendelea kulisaidia kwa hali na mali kadri uwezo utakavyoniruhusu”,alisema na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi.

Dewji alisema nia yake ya kuomba ubunge huko nyuma,lengo ilikuwa na kutaka kushirikiana na wananchi kuliletea maendeleo jimbo la Singida mjini tu, na sio kujinufaisha binafsi.

”Jimbo sasa limepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta zote muhimu.Najua bado tuna mengi ya kufanya ya kimaendeleo kwa kizazi cha sasa na kile kijacho.Kwa hiyo sitowaacha,tutaendelea kushirikiana kuliendeleza jimbo la Singida mjini ili liwe mfano wa kuigwa na majimbo mengine katika masuala ya kimaendeleo”,alisema.

Baadhi ya wakazi wa jimbo la Singida mjini wamedai Dewji ataendelea kukumbukwa kwa miaka mingi ijayo, kutokana na tabia yake ya kuwapenda wananchi wote na hakuwa na chembe chembe ya ubaguzi.

“Binafsi sidhani kama jimbo letu hili litakuja kupata mbunge wa aina ya Dewji.Ukiacha misaada yake mikubwa kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya maji, afya, elimu na kilimo, Dewji amesaidia hata ujenzi wa misikiti na makanisa madogo na makubwa ya mjini Singida na yale ya vijijini”,alisema Limu Bunka.

Aidha,alisema Dewji amesaidia pia kugharamia matibabu ya baadhi ya wakazi ndani na nje ya mkoa na amegharamia masomo ya mamia ya wananfunzi ambao wazazi/walezi wao hawana uwezo.
_MG_2292
Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mjini (Mbunge Mstaafu), Mohamed Dewji akimwombea kura Mgombea Urais wa CCM Dkt. John Pombe Magufuli (hayupo pichani) kwa wananchi wa Singida na vitongoji vyake katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Peoples, mjini Singida, Dewji pia ametangaza kumuunga mkono aliyemrithi kiti chake cha Ubunge, Ndugu Mussa Sima.
IMG_4821
Mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Dkt John Magufuli akiwahesabia kupiga 'Push Up' wagombea ubunge Mwigulu Nchemba wa Iramba (kulia), Musa Sima (katikati) wa Singida Mjini na Lazaro Nyalandu wa Jimbo la Singida Kaskazini jana wakati wa mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Peoples mjini Singida.
IMG_4214
Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mjini (Mbunge Mstaafu), Mohamed Dewji akiteta jambo na Mgombea Ubunge jimbo la Kaskazini, Lazaro Nyalandu wakati wa mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Peoples mjini Singida.
IMG_4182
Mtoto ambaye hakufahamika mara moja jina lake, akimsikiliza mgombea urais kupitia CCM Dk.John Pombe Magufuli uliofanyika kwenye viwanja vya Peoples mjini hapa jana,huku kando kando yake kukiwa na ujumbe maalum kwa Dkt.Magufuli.
IMG_4268
Majembe yakiwajibika kwenye mkutano wa kampeni za urais CCM katika Uwanja wa Peoples mjini Singida. Kushoto ni Mwakilishi wa Modewjiblog Singida mjini, Nathaniel Limu pamoja na Ahmad Michuzi wa Michuzijr Blog.
IMG_4856
Wakazi wa Singida mjini wakicheza na kumshangilia aliyekuwa Mbunge wa Singida Mjini (Mbunge Mstaafu), Mohamed Dewji katika mkutano wa kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Magufuli uliofanyika kwenye uwanja wa Peoples, mjini Singida.
IMG_4860
Umati wa wanaSingida ukimshangilia aliyekuwa Mbunge wa Singida Mjini (Mbunge Mstaafu), Mohamed Dewji mara baada ya kumalizika mkutano wa kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Magufuli uliofanyika kwenye uwanja wa Peoples, mjini Singida.

No comments: