Tangazo

March 30, 2016

SERIKALI YAJIPANGA KUWASAIDIA WAKULIMA KUPAMBANA NA MABADILIKO YA TABIA YA NCHI

DSC_1667
Wageni rasmi katika mkutano huo, Wa kwanza kushoto ni Mtafiti kutoka Taasisi ya Mtandao wa Kutathimini Sera za Chakula, Kilimo na Maliasili (FANRPAN), Njongenhle Nyoni, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida na Mkuu wa Kitengo cha Mazingira kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bi. Shakwaanande Natai.

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imejipanga kuhakikisha inawasaidia wakulima kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yanaonekana kuendelea kuikabili nchi.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mazingira kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bi. Shakwaanande Natai alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) na Taasisi ya Mtandao wa Kutathimini Sera za Chakula, Kilimo na Maliasili (FANRPAN) ili kujadili mpango wa Kilimo Salama (CSA).

Bi. Natai alisema serikali inatambua uwepo wa mabadiliko ya Tabia ya Nchi na kwasasa tayari wataalamu wanafanya tafiti ili waone ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia wakulima kupambana na mabadiliko hayo.

Alisema kwa sasa bado wakulima wengi hawajafahamu kama kuna mabadiliko ya tabia ya nchi na hivyo wamekuwa wakitumia njia za asili lakini baada ya utafiti watapatiwa mbinu mpya za kupambana na mabadiliko ambapo wataweza kutumia njia za kisasa ambazo zinaonekana kuwa bora zaidi.

“Serikali inatambua na tunajipanga kuwasaidia wakulima, shida kwa sasa bado wakulima wengi hawajajua kama kuna mabadiliko ya tabia ya nchi lakini wataalamu wapo wanafanya tafiti baada ya hapo tutajua tunawasaidia vipi,

“Kwa sasa kinachoonekana ni kutokueleweka kwa hali ya hewa kama mafuriko kutokea lakini kwa kuwa bado hawajapatiwa elimu wanashindwa kutambua na bado wanatumia njia za asili, tutawapa mbinu mpya watafanya kwa pamoja na mbinu wanazotumia sasa za asili,” alisema Bi. Natai.

Aidha alieleza kuwa baadhi ya huduma ambazo watapatiwa wakulima baada ya kukamilika kwa tafiti ni pamoja na kupewa elimu ya kilimo cha umwagiliaji, mbegu za kisasa ambazo zinawahi kukomaa na dawa za kupambana na magonjwa.

Nae mtafiti kutoka FANRPAN, Njongenhle Nyoni alisema taasisi yake imefanya mkutano huo ili kuona ni jinsi gani wanaweza kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi katika nchi ambazo wanafanya kazi ambapo Tanzania ni mojawapo.

Alisema wao wanafanya tafiti kuona hali ilivyo na baada ya hapo wanatazama changamoto zilizopo katika kupambana na mabadiliko na wanatoa ushauri ni jambo gani linaweza kufanyika ili kuwezesha kufanikisha kufanyika Kilimo Salama (CSA).

“Tunakutana na watu kutoka asasi za kijamii na taasisi mbalimbali ili kuona ni jinsi gani CSA inaweza kufanya kazi vizuri hasa katika maeneo tunafanya nao kazi na hii sio Tanzania tu hata mataifa mengine kama Malawi tunalifanya hili,” alisema Nyoni.

Pia iliongeza kuwa malengo ya FANRPAN ni kusaidia wakulima kuondoka katika janga la umasikini lakini pia kuwepo kwa chakula kilicho katika hali ya usalama bila kuathiriwa na mabadiliko ya tabia ya nchi.
DSC_1664
Mshereheshaji wa mkutano huo akiwakaribisha wageni waalikwa kabla ya kufunguliwa rasmi kwa mkutano huo.
DSC_1671
Baadhi ya wageni waliohudhuria katika mkutano huo kujadili mpango wa Kilimo Salama (CSA).
DSC_1682
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida akitoa neno la ufunguzi.
DSC_1697 DSC_1701
Mkuu wa Kitengo cha Mazingira kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bi. Shakwaanande Natai akielezea Kilimo Salama (CSA).
DSC_1749
Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuendelea na mkutano huo.
DSC_1754
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Mazingira kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bi. Shakwaanande Natai.
DSC_1759
Karl Deering kutoka Taasisi ya CARE akizungumzia Mpango wa Kilimo Salama Afrika (ACSAA)
DSC_1769
Baadhi ya wageni katika mkutano huo wakichangia hoja
DSC_1772 DSC_1819
Washiriki wa mkutano wakiwa katika makundi kujadili kuhusu Kilimo Salama (CSA)
DSC_1823 DSC_1829 DSC_1914
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uwezeshaji wa ESRF, Doris Likwelile akifunga mkutano.

No comments: