SALAAM ZA RAMBIRAMBI MSIBA WA JOSEPH SENGA
Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa masikitiko na
mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha mmoja wa waandishi wa habari za picha
mwandamizi na mahiri nchini, Joseph Senga kilichotokea usiku wa jana
akiwa kwenye matibabu nchini India.
Kama
taasisi na kisha mtu mmoja mmoja kuanzia kwa wanachama na viongozi wa
chama kwa hatua ya sasa tumejikuta tumeishiwa maneno ya kusema kuhusu
kifo cha mwandishi huyu mwandamizi, lakini katikati ya mshtuko na
majonzi tuliyonayo, tunaweza kusema kuwa kifo cha Senga, hasa siku
kiliyotokea, kimedhihirisha jambo moja kubwa kuwa alikuwa SHUJAA WA
DEMOKRASIA NA HAKI.
Kifo cha Senga kimetokea siku ambayo kulikuwa na matukio makubwa mawili kuhusu demokrasia na haki nchini.
Kwanza,
wakati Senga anafariki usiku wa Jumatano, Julai 27, mchana wa siku hiyo
hiyo Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, ilikuwa imetoa hukumu ya kifungo cha
miaka 15 jela askari anayefahamika kwa jina la Pacificius Simon kwa
hatia ya kosa la kumuua bila kukusudia aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa
Kituo cha Channel ten, mkoani Iringa.
Matukio
hayo matatu; kuuwawa kwa Mwangosi, hukumu ya aliyemuua na kifo cha
Senga, yana uhusiano mkubwa wa karibu huku Senga akiwa katikati yake,
kwamba;
Picha zote ambazo hadi leo zinaweza
kupatikana dunia nzima kupitia mtandao wa intaneti zikionesha mauaji ya
kikatili aliyofanyiwa Mwangosi, kuanzia ile ambayo inaonesha kundi la
askari polisi likiwa limemzunguka Mwangosi huku mmoja wao akiwa
amemlenga kwa bunduki ya kulipulia mabomu ya machozi, hadi zile ambazo
zinaonesha mwili wa mwandishi Mwangosi ukiwa umefumuliwa na kutawanywa
vibaya baada ya kulipuliwa, huku nyingine ikimuonesha mmoja wa askari
akiugulia maumivu ya ‘bomu’ lililomuua Mwangosi, zilipigwa na Shujaa
Senga.
Kwa watu waliokuwepo siku ya tukio hilo
baya kuwahi kuikumba tasnia ya habari nchini, watakumbuka kuwa Senga
alipiga picha zile akiwa katikati ya mirindimo na moshi wa mabomu,
ngurumo za risasi za moto na kundi la askari wengi ambao walikuwa
wanazidi hata idadi ya wanachama na viongozi wa CHADEMA waliokuwa
wamekusanyika kwa amani kwenye ofisi yao kijijini Nyololo kabla
hawajavurugwa na Jeshi la Polisi likiongozwa na RPC Michael Kamhanda.
Picha
zile ambazo ziliiambia dunia nzima ukweli wa tukio hilo, ziliokoa watu
wengi na bila shaka zilisaidia kutotokea kwa jambo kubwa ambalo watawala
walishaanza kuonesha nia ya kulitekeleza, kupitia maofisa waandamizi wa
Jeshi la Polisi, makao makuu na mkoani Iringa, ambao walitaka kuonesha
kuwa CHADEMA ‘walijilipua’, ambapo maana yake ni kwamba wafuasi,
wanachama na viongozi wa CHADEMA walikuwa na milipuko au vitu vya namna
hiyo.
Pili; Senga amefariki siku ambayo
Watanzania bila kujali tofauti zao, wakiongozwa na CHADEMA walitangaza
Operesheni UKUTA ambayo moja ya malengo yake ni kupigania haki za
makundi mbalimbali ya Watanzania, wakiwemo waandishi wa habari dhidi ya
mifumo kandamizi inayolelewa na watawala kupandikiza mbegu za utawala wa
kidikteta nchini.
Kwa muda mrefu, kupitia
chombo chake alichokuwa akikifanyia kazi hadi mauti yanamkuta, Free
Media, CHADEMA kama inavyofanya kazi na waandishi wa habari wa vyombo
mbalimbali, ilikuwa ikishirikiana na Senga kikazi, huku naye akifanya
kazi yake kwa uwezo mkuwa, akizingatia miiko na misingi ya taaluma ya
uandishi wa habari, kwa weledi mkubwa.
Habari
picha zake mbalimbali ambazo zimekuwa zikidhihirisha ukongwe wake katika
tasnia ya habari, zikiwemo za matukio ya CHADEMA, zitakuwa historia
itakayotunza jina lake miongoni mwa waandishi mahiri nchini ambazo
waandishi chipukizi watajifunza.
Kwa masikitiko
makubwa, CHADEMA inatoa salaam za pole kwa familia ya marehemu, Mhariri
Mtendaji wa Kampuni ya Free Media, wafanyakazi wenzake, tasnia ya
habari nchini na Watanzania wengi walioguswa na msiba huo. Mwenyezi
Mungu awatie moyo wa ujasiri kuyakabili majonzi mazito ya kifo cha
mpendwa Senga.
Huyo ndiyo Joseph Senga. Shujaa wa demokrasia na haki. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema.
Imetolewa leo Alhamis, Julai 28, 2016 na;
Tumaini Makene
Mkuu Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
No comments:
Post a Comment