Tangazo

February 23, 2017

JUMIA TRAVEL YAZINDUA HUDUMA ZA NDEGE

 Ofisa Habari wa Kampuni ya Jumia Travel, Geofrey Kijangwa (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu kampuni hiyo kuzindua huduma za ndege. Kushoto ni Meneja Mkazi wa Kampuni hiyo, Fatema Dharsee. 
 Meneja Mkazi wa Kampuni hiyo, Fatema Dharsee akizungumza na wanahabari.

Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.


 Na Dotto Mwaibale

KAMPUNI ya Jumia Travel imetangaza kuwa imezindua huduma za ndege kwa ajili ya wasafiri, hatua ambayo itapelekea kutanua wigo wa huduma zake. 

Uzinduzi huu unakuja kipindi ambacho Kilele cha Mkutano wa Pili wa Masuala ya Anga Afrika ukifanyika nchini Rwanda. 

Kwa sasa mtandao huo nambari moja kwa huduma za hoteli barani Afrika unatoa huduma za ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na mashirika makubwa ya ndege yakiwemo Precision Air, Kenya Airways, Rwandair Express, Qatar Airways, Emirates, Ethiopian Airlines, South African Airways, KLM, Fly Dubai, Turkish Airlines, Air Arabia, Air Seychelles miongoni mwa nyinginezo.

“Hii ni hatua nyingine kwetu sisi tukiwa tunalenga kuwa wakala unayeongoza kutoa huduma za usafiri kwa njia ya mtandao Afrika, huku tukiwapatia wasafiri huduma za kipekee. Pia ni mpango wetu wa kutengeneza sehemu moja ya kukidhi huduma zote za usafiri ikitoa malazi, vifurushi vya huduma, na tiketi za ndege, zote zikiwa zinapatikana sehemu moja, katika jitihada za kurahisisha usafiri Afrika,” alisema Paul Midy - Afisa Mtendaji Mkuu wa Jumia Travel.

Jumia Travel itakuwa ikitoa huduma kwa kushirikiana na washirika tofauti akiwemo Amadeus. “Huduma hii (ambayo kwa sasa inapatikana kupitia travel.jumia.com/flights) inawawezesha wateja wetu kutafuta, kulinganisha, na kufanya huduma pamoja na kukata tiketi za ndege mtandaoni kwa urahisi moja kwa moja kupitia kampuni mbalimbali za mashirika ya ndege duniani,” aliongezea Midy.  

Uzinduzi huu unaongezea orodha ya huduma kwa wateja wengi wa Jumia Travel ambazo wanaweza kuzifanya wenyewe kwa ndani na nje ya nchi. Ikiwa ni 3% tu ya sehemu ya usafiri wa anga duniani, Afrika inaonyesha uwezekano mkubwa wa kukua miaka ijayo, hususani kutokana na kuongezeka kwa uhitaji wa watu wa daraja la kati na kukua kwa uchumi wa Afrika.

“Jumia Travel imedhamiria kuwekeza kwenye kwenye soko ambalo linachochea maendeleo ya sekta ya ukarimu barani Afrika. Kwa Shirika la Usafiri wa Anga la Kimataifa, (IATA) kutabiri ukuaji thabiti kwa 4.8% kwenye idadi ya abiria barani Afrika ndani ya miaka 5 ijayo, hii inathibitisha tulivyojizatiti kimikakati kwa kutoa huduma zisizo na ukomo kwa wasafiri,” alimalizia Midy.

Naye kwa upande wake Meneja Mkaazi wa Jumia Travel Tanzania, Fatema Dharsee ameendelea zaidi kwa kufafanua kuwa, “Uzinduzi wa huduma hii kwenye mtandao wetu ni kukidhi haja ya muda mrefu ya wateja wetu waliokuwa wakiulizia endapo tutaweka na huduma za ndege. Ilikuwa inawawia ugumu kufanya huduma za hoteli kupitia Jumia Travel na kisha kukata tiketi za ndege sehemu nyingine. Tunaamini huduma hii itafungua Tanzania duniani na kuileta dunia Tanzania, yaani mtu anaweza akafanya huduma za ndani au nje ya nchi kwa sehemu kama vile Dubai, India na Uingereza. Lakini pia huduma hii itahamasisha ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga nchini kutokana na mfumo kurahisishwa.”

“Huduma hii tuna uhakika kuwa itakuwa ni suluhisho kubwa kwa wasafiri ndani na nje ya nchi. Kwa sababu, msafiri atakuwa na uhuru wa kuchagua huduma aitakayo kutoka kwa shirika la ndege alitakalo papo hapo kutokana na orodha itakayojitokeza. 

Inamaanisha kwamba Jumia Travel tulichokifanya ni kuzileta huduma za usafiri wa anga kutoka kwenye mashirika tofauti ya ndege kuja sehemu moja kama tulivyofanya kwa hoteli. Msafiri hatokuwa na haja tena kuwasiliana na shirika la ndege au wakala bali yeye mwenyewe kupitia mtandao wetu kwenye kompyuta, tabiti (tablet) au simu anaweza kujihudumia,” alihitimisha Dharsee.

Hivi karibuni kampuni hiyo ilizindua ofa za msimu wa sikukuu ili kuhamasisha utalii wa ndani barani Afrika. Kwa kuhusisha huduma za ndege ndani yake, Jumia Travel itaendelea kuunga mkono jitihada za kuzifikia sehemu mbalimbali za Afrika na nyinginezo duniani, wakati huo huo ikiwa na nia ya dhati ya kuendelea kutoa suluhisho la huduma kwa usafiri.

No comments: