Na Mathias Canal, Lindi
Baada ya kuimarisha umoja na ushirikiano wa wakulima
wenyewe ni vema wakulima wakajenga mahusiano mazuri na wafanyabiashara ili
kutokutoa mianya kwa madalali ambao mara nyingi wamekuwa wakilalamikiwa kuwa
wananunua mazao ya wakulima kwa bei ya chini huku wao wakiyauza kwa bei ya juu.
Hayo yameelezwa na baadhi ya wadau wa kilimo
waliozuru katika sherehe za maonesho ya Wakulima Kitaifa yanayofanyika katika
viwanja vya Ngongo Mkoani Lindi.
Wamesema kuwa Ni vema kukatengenezwa mfumo mzuri
utakaowasaidia wakulima kupata taarifa sahihi za masoko na bei halisi ya bidhaa
kupitia umoja wao, kuliko kuendelea kusherehekea kila mwaka wakati wakulima
bado wanateseka na bei kandamizi za madalali.
Suala hili linaenda sambamba na kaulimbiu ya sherehe
za Nane Nane mwaka huu ambayo ni “Zalisha kwa Tija Mazao na Bidhaa za
Kilimo Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati”
Juma Msembi ni moja ya washiriki wa Maonesho ya
Nanenane anasema serikali inapaswa kuzidi kuwa kiunganishi kizuri kati ya
wakulima na soko, ili wakulima wasikate tamaa katika kuzalisha chakula kingi.
Anasema kuwa anaamini Sherehe hizi zitakuwa chachu
ya kujadili na kutathmini maendeleo ya sekta ya kilimo na changamoto zinazowakabili
wakulima na kuangalia namna ya kuzitatua.
Katika Maonesho haya wakulima watajifunza mbinu bora
za kisasa za kilimo zitakazowawezesha kupata mazao mengi na kuinua kipato chao.
Msembi anatoa wito kwa wakulima na mashirika
kujitokeza katika maonesho hayo kwa sababu watapata fursa ya kujifunza mambo
mengi na kubadilishana uzoefu na wataalamu mbalimbali wa kilimo.
No comments:
Post a Comment