Tangazo

September 11, 2017

MJI MKONGWE WA ZANZIBAR: PALE DUNIA YA KALE INAPOKUTANA NA YA KISASA

Na Jumia Travel Tanzania

Miongoni mwa majengo yake mengi yakiwa yamejengwa mnamo karne ya 18 na 19, Mji Mkongwe wa Zanzibar bado haujapoteza taswira yake halisi mpaka hivi leo. Na kutokana na muonekano huo, kutembea na kuvinjari mitaa na majengo mbalimbali kunakufanya ujihisi kama kweli ulikuwepo kipindi cha nyuma pindi inajengwa.
Kati ya majengo maarufu ambayo Jumia Travel inakuhakikishia utayaona pindi utakapoingia kwenye mji huu ni pamoja na Ngome Kongwe iliyojengwa kwenye eneo la mwanzo la Kanisa la Wareno; nyumba ya maajabu; kasri kubwa iliyojengwa na Sultan Barghash; zahanati ya kale; Kanisa Kuu Katoliki la Mtakatifu Joseph; Kanisa Kuu la Kristu la Waanglikana likiwa limejengwa kukumbuka kazi ya David Livingstone katika kukomesha biashara ya utumwa na kujengwa eneo lilipo kuwepo soko la watumwa; makazi ya aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa watumwa Tippu Tip; Msikiti wa Malindi Bamnara; jengo la Jamat Khan lililojengwa kwa ajili ya dhehebu la Ismailia; eneo la makaburi ya Kifalme; na mabafu ya Kiajemi.
Kwa pamoja, mitaa na barabara nyembamba zikiwa na kona nyingi, na majengo makubwa yanayotazamana na bahari ndyo yanaufanya mji huu kuwa wa kipekee ukiakisi shughuli za muda mrefu za kibiashara kati ya Waafrika na Waarabu. Kwa ujumla, Mji Mkongwe unatambulika kama sehemu ambayo hatimaye biashara ya utumwa ilikomeshwa.

Kutokana na upekee na umaarufu wake mamia ya maelfu ya watalii kutoka kona mbalimbali za dunia husafiri kuja kujionea vivutio vya kila aina vinavyopatikana kwenye mji huu mkongwe wa Zanzibar.

Kwa ufupi takribani kila kitu ndani ya Mji Mkongwe kina historia ya kuvutia na kusisimua. Kuanzia mila na tamaduni za watu wake, shughuli wanazozifanya, vyakula vyao na majengo ni utalii tosha ambao hauwezi kupatikana sehemu yoyote duniani.
Huchukua muda wa saa moja na nusu kusafiri kwa kutumia boti kutoka Dar es Salaam mpaka kufika Zanzibar na usafiri huanzia saa moja asubuhi mpaka saa 12 za jioni. Hivyo basi kumbe inawezekana kwa mtu kutokea jijini Dar es Salaam akaenda kule, akatalii na kurudi siku hiyo hiyo. Na kama una mpango wa kuufaidi zaidi mji huo pia inawezekana kwani vyakula na malazi vya gharama nafuu kabisa ambayo kila mtu anaweza akamudu.
Uzuri wa Mji Mkongwe ni kwamba ni rahisi kuuzunguka kwani mitaa yote inapitika kwa urahisi kabisa aidha kwa kutumia ramani ya karatasi au simu (google map) au muongozaji wa kitalii utayempata. Ni vizuri kuwa na muongozaji mzuri kama ni mara yako kwanza kufika kule ili iwe rahisi na pia kutembelea sehemu nyingi zaidi ambazo hauzifahamu.

Kikubwa cha kushangaza zaidi ni namna majengo yalivyojengwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia vifaa mbalimbali kama vile chokaa, matumbawe na miti. Na cha kuvutia zaidi ni umri wa majengo hayo ambayo yamekuwepo karne na karne bila ya kupoteza uhalisia wake. Pongezi kubwa ziende kwa serikali na shirika la Umoja wa Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kuweka jitihada kubwa na sheria za kuulinda mjii huu. Kutokana na jitihada hizo mnamo mwaka 2000 UNESCO liliutangaza Mji Mkongwe wa Zanzibar kama eneo la urithi wa dunia. 
Utakuwa haujaufaidi Mji Mkongwe endapo hautopata fursa ya kula vyakula mbalimbali (vya baharini) vinavyopatikana katika migahawa tofauti. Eneo maarufu ambalo unaweza kuvipata vyakula vya aina hiyo kwa pamoja ni kwenye bustani ya Forodhani. Litakuwa jambo la ajabu kama umefika Zanzibar na hukuenda kutembelea eneo hili. Umaarufu wa bustani ya Forodhani umetokana na mkusanyiko wake wa aina lukuki za vyakula vya baharini vinavyopatikana pale kila siku kuanzia jioni. Na ni eneo ambalo huwakutanisha watu kutokea sehemu mbalimbali za visiwa vya Zanzibar, hivyo inawezekana kukutana na watu ambao mlikuwa mkipishana mchana kutwa.

Kutembelea, kuogelea na kutazama jua likizama kwenye fukwe ya bahari ya Hindi ukiwa Zanzibar nazo ni miongoni mwa shughuli ambazo watalii wengi hufurahia. Baadhi ya hoteli ambazo ukiwa kwenye Mji Mkongwe unaweza kuyafanya hayo ni kama vile Mizingani Seafront Hotel, Africa House Hotel na Seyyida Hotel & Spa.

Kwa kumbukumbu zako itakuwa ni vema zaidi ukibeba kamera kwa ajili ya kupiga picha matukio mbalimbali unayoyaona njiani. Kwa majengo inakuwa ni rahisi zaidi ila kwa watu itakuwa ni busara ukaomba ruhusa ili kuepuka matatizo kwani sio wote watakuwa tayari kufanya hivyo. Zanzibar ni kubwa na ina maeneo mengi ya kutembelea ila kwa leo Jumia Travel inaamini angalau utakuwa umeipata picha ya Mji Mkongwe wa Zanzibar na shughuli za kufanya na kufurahia ukiwa kule.

No comments: