Na Hamza Temba - Wizara ya Maliasili
..........................................................................
Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga amesisitiza agizo la Serikali lililotolewa
hivi karibuni na Waziri Mkuu kuhusu kukamilisha zoezi la uwekagi wa vigingi vya
mpaka kwenye maeneo ya hifadhi nchini ifikapo Desemba 31 mwaka huu.
Amesema lengo la kukamilisha
zoezi hilo ni kuiwezesha Serikali kufanya uamuzi wa mwisho wa kumaliza migogoro
ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu baina ya vijiji na maeneo ya hifadhi nchini.
Mhe. Hasunga ametoa
kauli hiyo jana wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi ya msitu wa
Isalalo Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe ambapo aliziagiza taasisi zilizo chini ya
Wizara yake kukamilisha zoezi hilo kabla ya tarehe hiyo ili kuiwezesha Serikali
kubaini maeneo yenye mapungufu na kuyatolea uamuzi.
“Ifikapo tarehe 31
tuwe tumemaliza kuweka hizo beacon (vigingi) za mipaka, baada ya hapo hatua
itakayofuata, Serikali tutakaa na kuangaliza ni vijiji vingapi au maeneo gani
yameingia ndani ya hifadhi, tuangalie je tuwaachie hayo maeneo wananchi au
tuwahamishe tuwapeleke maeneo mengine, maamuzi hayo yatakuja baada ya kufanya
tathmini na kubaini penye mapungufu.
“Sasa ikitokea kwamba
imefika tarehe 31 hatujatekeleza hili mimi kama Naibu Waziri nitakuwa sina
kazi, maana sijatekeleza agizo la Serikali, kwahiyo lazima tulisimamie, na mimi
sasa kabla halijanipasukia nitakupasukia bwana Meneja (Meneja TFS Wilaya ya
Mbozi), nitakuja kukagua mipaka, na kabla ya tarehe 31 nitakuja kukagua tena,”alisema
Naibu Waziri Hasunga.
Wakati huo huo
amekemea vitendo vya baadhi ya wananchi wanaoingiza mifugo kwenye maeneo ya
hifadhi nchini na kuwataka kufugia majumbani kwao au maeneo yaliyotengwa kwa
ajili hiyo, amewatahadharisha pia juu ya ukali wa sheria za uhifadhi na kwamba
endapo mifugo itakamatwa hifadhini sheria zilizopo zinaruhusu utaifishaji.
Aidha aliwataka
wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo ya msitu wa Isalalo kuacha vitendo vya
uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti hovyo kwa ajili ya mkaa na
uanzishaji wa maeneo ya kilimo. Pia alitoa wito kwa wananchi kulinda vyanzo vya
maji na kuacha vitendo vya uchomaji moto misitu.
Katika hatua nyingine ameuagiza uongozi
wa Wakala wa Huduma za Misitu Nyanda za Juu Kusini kuwashirikisha wananchi wanaoishi
jirani na hifadhi hiyo ya msitu kwenye ulinzi wa hifadhi ikiwa ni pamoja na
kuwawezesha miche ya miti ya kutosha kwa ajili ya kupanda kwenye maeneo
yao yanayozunguka hifadhi hiyo.
Aidha ameuagiza uongozi wa halmashauri
ya wilaya ya Mbozi kupima maeneo yao na kuweka mpango bora wa matumizi ya ardhi
kwa kuanisha maeneo kwa ajili ya kilimo, ufugaji na maeneo ya hifadhi ili
kuepusha migogoro isiyo ya lazima ya wananchi.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa
Huduma za Misitu Wilaya ya Mbozi, Fred Mgeni alisema katika kuimarisha mpaka wa
hifadhi ya msitu huo wa Isalalo ambao una ukubwa wa hekta 11,552, jumla ya
vigingi 30 vimewekwa kuzunguka hifadhi hiyo.
Alizitaja baadhi ya changamoto
katika hifadhi hiyo kuwa ni uvamizi wa wakulima na wafugaji, uvunaji haramu wa
miti, uchomaji mkaa na moto, na ung'oaji wa vigingi vya mpaka na mabango.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo
alisema ili kuimarisha uhifadhi wa msitu wa Isalalo ni vema wananchi
wakashirikishwa ikiwemo kuanzishwa kwa vikundi vya vijana ambao watawezeshwa
bodaboda zitakazowanufaisha kiuchumi na wakati huo huo zikatumika kwenye ulinzi
wa hifadhi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kushoto) akioneshwa ramani ya Hifadhi ya Msitu wa Isalalo na Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Wilaya ya Mbozi, Fred Mgeni (kulia) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua hifadhi hiyo kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi mkoani Songwe jana.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo wakati wa kukagua Hifadhi ya Msitu wa Isalalo Mkoani Songwe kwenye ziara yake ya kikazi ya kuimarisha uhifadhi mkoani humo jana.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na Mkuu wa Wilaya Mbozi, John Palingo (kushoto) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua Hifadhi ya Msitu wa Isalalo uliopo wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi mkoani humo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kulia) akimsikiliza Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Wilaya ya Mbozi, Fred Mgeni (kulia) wakati akikagua Hifadhi ya Msitu wa Isalalo uliopo wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuimarisha uhifadhi mkoani humo jana. Wa tatu kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, John Palingo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Malolo wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuimarisha uhifadhi mkoani humo jana, alikagua Hifadhi ya Msitu wa Isalalo na kuagiza zoezi la uwekaji vigingi vya mpaka likamilike ifikapo Desemba 3l.
No comments:
Post a Comment