Tangazo

January 22, 2018

Kamal yaleta tabasamu la mwaka mpya kwa wenye ulemavu Dar kupitia mradi wa viungo

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) Anthony Mavunde akikabidhi miguu bandia kwa baadhi ya watu wenye ulemavu ambayo ni msaada uliotolewa na kampuni ya Kamal Group ya Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kutoka kushoto ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya  Dar es Salaam, Dk. Coretha Komba, Mkurugenzi wa Kamal Group Satyam Gupta, Mwanzilishi wa Kamal Group Santosh Gupta, Mwenyekiti wa Kamal Group Gagan Gupta naMkurugenzi Sameer Gupta. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Baadhi ya watu wenye ulemavu wakijaribisha miguu bandia baada ya kukabidhiwa kwao na kampuni ya Kamal Group ya Dar es Salaam katika hafla iliyofanyika jijini mwishoni mwa wiki. Hafla ya kukabidhi miguu hiyo bandia ilihidhuriwa na Naibu Waziri kutoka katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) Anthony Mavunde (hayupo pichani). 

Baadhi ya watu wenye ulemavu wakishangilia baada ya kukabidhiwa miguu bandia kutoka kwa kampuni ya Kamal Group ya Dar es Salaam katika hafla iliyofanyika jijini mwishoni mwa wiki. Hafla ya kukabidhi miguu hiyo bandia ilihidhuriwa na Naibu Waziri kutoka katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) Anthony Mavunde (hayupo pichani).
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Mwandishi wetu,

Dar es Salaam

ZAIDI ya watu wenye ulemavu mia moja wa jiji la Dar es Salaam - waliopoteza miguu yao kutokana na ajari na magonjwa - wataweza kutembea tena baada ya kampuni ya Kamal Group kuwaletea zawadi ya kudumu ya mwaka mpya.

Kupitia mfuko wake wa Peoples’ Empowerment Foundation (PEF), Kamal Group imetoa miguu bandia yenye thamani ya mamilioni ya fedha kwa watu 108.

Bei ya mguu bandia mmoja katika hospitali za rufaa hapa nchini huanzia kati ya Sh1 milioni hadi Sh3 milioni.

“Sina la kuwalipa ila itoshe tu kusema ninashukuru sana kwa msaada huu. Kwa sasa nitaweza kutembea na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda. 

Sijaweza kutembea tangu nilipopoteza mguu wangu mmoja mwaka 2009,” alisema Mwanaisha Mohammed.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo kwa wahusika, iliyohudhuriwa na Naibu Waziri kutoka katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) Anthony Mavunde, Mwenyekiti wa Kamal Group, Gagan Gupta alisemakampuni yake inaamini inao wajibu wa kusaidia maendeleo ya jamii inayoizunguka.

“Kamal Group inaamini katika falsafa ya kukua pamoja na jamii inayotuzunguka…tunaamini ni wajibu wetu kusaidia jamii inayotuzunguka na ni wajibu wetu kuleta tabasamu katika nyuso za watu kuhakikisha wale wenye ulemavu wa miguu wanaweza kutembea tena na kusadia katika kuijenga Tanzania yenye viwanda,” alisema Gagan Gupta na kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Makonda, kwa kusaidia kuwaleta watu wenye ulemavu wanaohitaji msaada huo

Alisema ilianzisha mradi wa kutengeneza na kugawa bure miguu bandia miaka mitatu iliyopita na mpaka sasa wananedelea kuifanya.

Naye Naibu Waziri Mavunde alisema kampuni hiyo imejidhilisha ni rafiki wa kweli wa Watanzania na hatua kama hizo zinaifanya Serikali kuzidi kufikiria jinsi ya kuboresha zaidi mazingira ya kufanya biashara nchini. 

“Kama serikali, tutafurahi zaidi endapo kampuni nyingi zaidi zitaweza kuiga mfano huu na kwa kufanya hivyo, tutapata nguvu zaidi katika kuboresha zaidi mazingira ya biashara nchini,” alisema Mavunde.

Tanzania inakadiriwa kuwa na watu 3.6 milioni wenye ulemavu ambapo kati yao, 1.7 milioni wanahitaji viungo bandia. 

Mpaka sasa, takwimu za Chama Cha Walemavu Tanzania (Chawata) zinaonyesha ni asilimia 20 tu ndiyo wenye uwezo wa kupata viungo bandia huku wengi wakilazimika kutembelea magongo ili kuweza kushiriki katika ujenzi wa taifa.

No comments: