Wakurugenzi
Watendaji wa Kampuni ya Spash International Co Ltd Shafeek Purayil (kulia)
na Japhet Alexander wa Kampuni ya Kamanda Security Guard Co. Ltd, wakipelekwa
mahabusu ya Mahakama ya kisutu jijini Dar es Salaam leo Februari 19, 2018 baada
ya kusomewa mashtaka mawili ya jinai kwa kushindwa kujisajili na Mfuko wa Fidia
kwa Wafanyakazi, (WCF), na kuwasilisha taarifa za shughuli za Makampuni
wanayoyaongoza kwa Mfuko huo. Washtakiwa wakipatikana na hatia wanakabiliwa na
kifungo kisichopungua miaka mitano (5), jela au faini isiyozidi shilingi
milioni hamsini au vyote kwa pamoja.
K-VIS BLOG
MFUKO wa Fidia Kwa
Wafanyakazi (WCF), umewafikisha mahakamani waajiri wanne (4) kwa kushindwa
kujisajili na Mfuko huo.
Waajiri hao ambao ni Wakurugenzi
Watendaji, wamefikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijinin Dar es
Salaam, leo Februari 19, 2018 wakikabiliwa na makosa mawili kila mmoja.
Kwa mujibu wa Mwendesha
Mashtaka wa Serikali Bw. Emilly Kiria, washtakiwa ni pamoja na Bw.Riziki Silas
Shemdoe na Bw. Deusdedit Samwel Kibassa ambaye hakuwepo mahakamani na
aliwakilishwa na wakili na wote wanatoka Kampuni ya ENCC CONSULTANTS na wengine ni Wakurugenzi
Watendaji wa Kampuni ya SPASH INTENATIONAL CO. LTD, Malakkara P,
Semis na Shafeek M. Purayil. Wengine ni Wakurugenzi Watendaji wa LASAR
LOGISTIC, Abshir Farah Gure na Farhiya Hersiwarsame, wakati Mshtakiwa
mwingine ni Bw.Josephat Alexander ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya KAMANDA
SECURITY GUARDS CO. LTD.
Akisoma mashtaka mbele
ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, Bi.Victoria
Nongwa, Mwendesha Mashtaka wa Serikali Bw. Emily Kiria, alisema waajiri hao wametenda
makosa mawili ambayo ni kushindwa kujisajili na kuwasilisha taarifa za
shughuli wanazozifanya kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi,
ambapo ni kinyume cha Kifungu cha 71 (1)
(a) na 71 (4) cha Sheria ya Fidia Kwa Wafanyakazi Sura ya 263 marejeo ya mwaka
2015.
Kosa la pili ni
kushindwa kutoa taarifa kwa Afisa wa Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi ambapo ni
kinyume na Kifungu cha 8 (5) (c), kikisomwa pamoja na Kifungu cha 96 cha Sheria
ya Fidia Kwa Wafanyakazi Sura ya 263 marejeo ya mwaka 2015.
Kabla ya Mfuko kuchukua hatua hii ya kuwafikisha mahakamani, washtakiwa walipewa taarifa ya
kutekeleza takwa hilo la kisheria katika tarehe mbalimbali, kati ya Septemba
2017 hadi Januari 2018 lakini walishindwa kutekeleza.
Washtakiwa hao endapo
watapatikana na hatia wanakabiliwa na kifungo kisichozidi miaka 5 jela au faini
isiyozidi shilingi milioni 50 au vyote kwa pamoja.
Akizungumza na
waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo, Meneja Matekelezo (Compliance
Manager), wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi,
(WCF), Bw. Victor Luvena alisema hatua hii ya kuwapandisha kizimbani waajiri
hao ni mwanzo tu na kwamba Mfuko utachukua hatua kama hiyo kwenye mikoa yote
Tanzania Bara.
“Ninawaasa waajiri
kutoka sekta ya umma na binafsi, Tanzania Bara, kutekeleza takwa hili la
kisheria kwa kujisajili na Mfuko ili kutimiza wajibu wao ili kuepuka shuruti.”
Alisema.
Shafeek Purayil(mbele) na Japhet Alexander wakitoka mahakamani baada ya kusomewa mashtaka na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Bibi Victoria Nongwa |
Shafeek Purayil
Meneja Matekelezo (Compliance Manager), wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw.
Victor Luvena akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo. Alisema washtakiwa wengine Zaidi watapandishwa kizimbani Jumanne Februari 20, 2018 kwa makosa hayo hayo. Kulia ni Mwanasheria wa WCF, Bw. Deo Ngowi.
No comments:
Post a Comment