Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya
Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori nchini (TAWA), Meja Jenerali mstaafu
Hamisi Semfuko (wa pili kushoto mwenye miwani), akizungumza na walinzi wa
wanyamapori katika maeneo yanayozunguka Pori ya Akiba la Maswa mkoani Simiyu alipokua akikagua shughuli za uhifadhi na
ulinzi katika maeneo hayo juzi.
Xxxxxxxxxxxx
MARA
WALINZI wa wanyamapori katika maeneo yanayozunguka Pori ya Akiba la Maswa yanayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wametakiwa kuwa makini na waadilifu kutokana na kuongezeka kwa wanyama adimu wanaofika maeneo yao.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa
Bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori nchini (TAWA) Meja
Jenerali mstaafu Hamisi Semfuko alipokua akikagua shughuli za uhifadhi na
ulinzi katika maeneo hayo.
Meja Jenerali Semfuko, alisema kazi
ya kupambana na ujangili inahitaji uvumilivu, uadilifu na ujasiri mkubwa
kutokana na mazingira hatarishi yaliyopo.
"La muhimu kuna taatifa maeneo
haya wameanza kuja wanyama adimu hivyo ningependa muongeze jitihada hizi mara
dufu wanyama hao wasidhurike," alisema.
Katika ziara hiyo wajumbe wa Bodi ya
TAWA walipokea taarifa ya timu ya pamoja kati ya TAWA, Mamlaka ya Hifadhi za
Taifa (TANAPA), Frankfurt Zoological Society ( FZS), TAWIRI na Friedkin
Conservation Fund (FCF) katika kuhifadhi na kulinda na kuhifadhi wanyama adimu.
Taarifa hiyo iliyowasilishwa na
wataalamu Philbert Ngoti wa TANAPA na Gerald Nyaffi wa FZS katika eneo la
kitalu kilichopo Maswa Mbono kinachoendeshwa na kampuni ya Tanzania Game
Tracker Safaris (TGTS).
Wataalam hao walisema wamefanikiwa
katika mradi huo kwa ufadhili wa familia ya Friedkin inayomiliki TGTS
ililiyofadhili fedha, vifaa pamoja na helikopta, kazi ijayotarajiwa kuendelea
katika maeneo mengine.
Katika ziara hiyo TAWA
imeridhishwa na utendaji wa Makampuni ya uwindaji na upigaji picha za kitalii,
yaliyopo katika maeneo yake kwa kusimamia uhifadhi na ulinzi pamoja na
kuchangia miradi ya maendeleo ya wananchi yenye thamani zaidi ya sh 40 bilioni.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (TAWA), Dk James Wakibara akizungumza
na waandishi wa habari juu ya mchango kwa jamii, uhifadhi na kiuchumi wa
makampuni ya uwindaji wa kitalii zilizowekeza katika maeneo yao.
Maeneo yaliyotembelewa na TAWA ni
pamoja na Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori(WMA) ya Makao wilayani Meatu
inayosimamiwa na kampuni ya Mwiba Holdings Limited.
Dk Wakibara alisema, licha
mchango wa makampuni kwenye jamii, pia TAWA kupitia malipo ya kampuni
hizo, imekuwa ikitoa takriban sh 6.5 bilioni kila mwaka kwa vijiji vyenye
wawekezaji hao na halmashauri.
Makampuni hayo yamewekeza katika
baadhi ya maeneo ya vitalu 159 vilivyopo nchini na maeneo ya
hifadhi za jamii za wanyamapori (WMA) 38 zilizopo nchini.
"Hizi kampuni za kitalii zina
mchango mkubwa sana pia katika uhifadhi wa maeneo haya, hasa katika vita dhidi
ya ujangili ikizingatiwa asilimia 95 ya maeneo yaliyohifadhiwa nchini yapo
chini ya TAWA"alisema
Alisema kwa sasa mapato ya TAWA
kutokana na shughuli za uhifadhi, yamefikia dola milioni 20 lakini kuna mikakati ya
kuongeza mapato hayo mara nne zaidi hadi kufikia dola milioni 80.
"kuna dhana potofu kuwa uwindaji
wa kitalii ni kumaliza wanyama hili sio kweli, kwani haya makampuni hayajawahi
kufikia hata robo kiwango cha kuwinda wanyama ambacho kinatolewa kila
mwaka na TAWA na mashirika ya kimataifa"alisema
Mwenyekiti wa bodi ya TAWA, Meja
Jenerali mstaafu Hamisi Semfuko alisema mamlaka hiyo ipo katika
mabadiliko makubwa ili kuhakikisha jamii inanufaika zaidi ya uhifadhi wa
wanyamapori,katika kusaidia miradi ya kijamii ya maji, afya Elimu na uhifadhi.
Mwenyekiti huyo na bodi yake ambao
walitembelea pori la Makao, lilipo mpakani mwa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro
na Meatu,alisema wameridhishwa na utendaji wa kampuni ya Mwiba Holding katika
eneo hilo.
No comments:
Post a Comment