Tangazo

October 31, 2011

Wake wa Viongozi wa Jumuia ya Madola washiriki mkutano wa CHOGM 2011

Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda – Perth, Australia
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ni mmoja wa wake wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuia ya madola waliohudhuria mkutano wa siku tatu wa jumuia hiyo unaofanyika mjini Perth nchini Australia.
Wake hao wa viongozi  walishiriki ufunguzi wa mkutano huo uliofunguliwa  na Malkia Elizabeth wa pili na baada ya ufunguzi waliweza kuendelea na ratiba yao ya kujifunza na kujadili mambo mbalimbali yanayaikabili jamii inayowazunguka ikiwa ni pamoja na afya, elimu, utamaduni, mila na michezo.
Baada ya kumalizika kwa ufunguzi huo walianza ratiba yao kwa kusikiliza mada  kuhusu afya ya binadamu  ilitolewa na Kanali Dk. Robert Walters ambaye ni  Balozi wa Serikali wa afya ya binadamu na Julian Krieg Afisa mtendaji  na mwalimu wa jamii  katika mpango wa mkoa wa Afya ya binadamu.
Mme wa Waziri Mkuu wa Australia Tim Mathieson aliweza kuwatembeza wake hao wa viongozi maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na makumbusho ya Australia’s Aboriginal and Torres Strait Islander ambako waliweza kujifunza historia ya nchi hiyo pamoja na utunzaji wa mila na utamaduni wao.
“Asili ya wenyeji wa nchi hii  ni watu weusi ambao kwa sasa kizazi chao kinatishia kumalizika  kutokana na uchache wao lakini miaka ya nyuma  Waingereza walihamia  hapa  na kuzaliana na hivyo idadi yao kuwa kubwa kuliko wenyeji hivi sasa asilimia kubwa ya waustralia ni watu weupe.
Nchi hii inaongozwa na waziri mkuu Julia Gillard’s huku  mtalawala wa nchi akiwa  ni Malkia wa Uingereza Elizabeth wa pili”, alisema Mathieson.
Katika makumbusho hayo pia walijifunza mila za watu wa Magharibi ya Australia  ambao wanaishi kandokando ya Bahari ya Hindi hivyo walifahamu  utawala wao, faida wanazozipata hususani za kibiashara  na utalii kutokana na  matumizi ya bahari na bandari ambayo ni lango kuu la meli.
Waliweza kutembelea bahari ya Hindi na kujionea shughuli za biashara na utalii zinavyofanyika katika ukanda wa pwani, meli kubwa za mizigo zinavyotia nanga, kupakua na kupakia  mizigo na kuona jinsi maaandalizi ya mashindano ya kimataifa ya  mchezo wa mashua (Sailing World Championships) yanayotarajia kufanyika katika mji huo mwishoni mwa mwaka huu yanavyoendelea.
Wake hao wa viongozi walishukuru kwa ziara na mafunzo waliyoyapata na kusema kuwa yatawasaidia katika kazi zao wanazozifanya kila siku ikiwa ni pamoja na kuboresha afya ya mama na mtoto na elimu ya mtoto wa kike.

No comments: