Tangazo

November 7, 2011

SHULE YA SEKONDARI YA WAMA - NAKAYAMA YAPEWA MSAADA WA VITABU 1000

Mama Salma Kikwete akiwa na Princess Camila.
Na Anna Nkinda – Maelezo

Shule ya Sekondari ya wasichana ya WAMA-NAKAYAMA iliyopo Rufiji mkoani Pwani imepokea msaada wa vitabu 1000 kutoka kwa Taasisi ya  British Charity READ International ambayo inafanya kazi ya kukusanya vitabu nchini Uingereza na kuvigawa katika nchi za Afrika.

Vitabu hivyo vimekabidiwa leo kwa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Mendeleo (WAMA) inayomiliki  shule hiyo na Hana Mitchell Mtendaji mkuu wa shirika hilo mbele ya Duchess of Cornwall  Camila Parker Bowles katika viwanja vya WAMA jijini Dar es Salaam.

Akikabidhi vitabu hivyo Mitchell alisema kuwa Read International na vijana wake 1000 wamekuwa wakitoa material ya elimu kwa zaidi ya vijana nusu milioni  ndani ya  shule 1000 katika mikoa 14 hapa nchini kwani kupatikana kwa elimu kunamsaidia mtu kupiga mbele hatua moja na hivyo  na kujikwamua na umaskini.

“Kuwepo kwenu hapa kunaonyesha kazi kubwa ya watu wanaojitolea katika Nchi za Tanzania na Uingereza  kwani nchini Tanzania  wanafunzi wanachangia kusoma kitabu kimoja lakini Taasisi yetu  inafanya kazi ya kuhakikisha kuwa  inatoa vitabu viwili   kwa kila mtoto aliyeko shuleni ambaye  atavisoma na kuvifurahia”, alisema Mtendaji Mkuu wa Read International.

Aliendelea kusema kuwa  vijana kutoka Tanzania na Uingereza wanafanya kazi kwa pamoja ya kubadilisha maisha yao kwa kitabu kimoja kuweza kuondoa ujinga kwa vijana zaidi ya 1000 kwani wanaondoa tofauti kwa vijana hao kwa kuwapa nafasi mbalimbali.

Kwa upande wake mke wa Rais Mama Salma Kikwete aliishukuru Taasisi hiyo kwa kuwa washirika wakubwa wa kuboresha elimu kwa miaka mingi na kuhakikisha kuwa vitabu vinapatikana kwa watoto wa Tanzania.

Mama Kikwete alisema, “Vitabu tulivyovipata leo vitawaongezea ujuzi wanafunzi wetu wa WAMA-NAKAYAMA kwani ninauhakika  kuwa vitawasaidia kufahamu mambo mbalimbali katika masomo yao na tutavitumia kwa manufaa ya shule yetu”.

Mama Kikwete alikabidhiwa kitabu kimoja na Princess Camila kitabu ambacho kilikamilisha jumla ya vitabu milioni moja  vilivyotolewa na Read International ambayo ni taasisi ndogo ya kujitolea ya Waingereza inayofanya kazi ya kukusanya vitabu kupitia maelfu ya vijana wanaojitolea na kuvisambaza katika shule  mbalimbali hapa nchini.

Duchess of Cornwall  Camilla alikutana  na wanafunzi walionufaika na mradi huo kutoka shule ya Sekondari ya Kilakala pamoja na wanafunzi watakaonufaika na mradi huo kutoka shule ya Sekondari ya wasichana ya WAMA – NAKAYA.

Camila ameambatana na mme wake Prince Charles katika ziara yao ya siku nne ya kutembelea  Tanzania.

No comments: