Tangazo

April 18, 2012

SERIKALI YA TANZANIA IMEPIGA HATUA KUBWA KATIKA MPANGO WA OPG

Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia katika ukumbi wa mikutano wa Brasilia Convention Centre jijini Brasilia, Brazil, April 17, 2012 katika mkutano wa Open Government Partnership.

Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa meza kuu na mwenyeji wake Rais wa Brazil Mama Dilma Rousseff  na wajumbe wengine katika ukumbi wa mikutano wa Brasilia Convention Centre jijini Brasilia, Brazil, April 17, 2012 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Open Government Partnership. Kulia ni Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani Bi Hilary Clinton.
 
***************************

Serikali ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutekeleza mpango wa ubia wa uwazi serikalini (Open Government Partnership-OPG) kama ilivyoahidi katika kikao kilichopita Disemba 2011.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameeleza hatua zilizofikiwa jana tarehe 17 April, 2011 katika kikao cha kwanza cha viongozi wa juu kinachofanyika Brasilia, Brazil. Katika kikao hicho, Rais Kikwete pamoja na viongozi wengine kutoka Marekani, Georgia na mwenyeji Brazil wametoa hotuba za ufunguzi.

Baadhi ya hatua ambazo serikali imepiga katika ubia wa uwazi serikalini ni pamoja na shughuli za bunge la Tanzania kuendeshwa kwa uwazi na kutangazwa moja kwa moja na vyombo vya habari.

"Watanzania wanapata fursa ya kuona wawakilishi wao wakijadili na kuuliza maswali kutoka serikalini , bajeti za serikali zinapitiwa na kujadiliwa na Kamati za Bunge na Bunge kwa ujumla, uhuru mkubwa wa vyombo vya habari na kuwekwa wazi kwa shughuli za Mkaguzi Mkuu wa Serikali ambapo ripoti hutolewa na kujadiliwa kwa uwazi na Bunge" Rais ameeleza kuwa tayari Tanzania imeanza kuziangalia  upya sheria za uhuru wa kupata habari, vyombo vya habari na sheria za kutangaza mali kwa maafisa wa Serikali.

Rais Kikwete amewambia wajumbe wa mkutano kuwa yeye na Serikali yake ni waumini wakubwa wa ushirikishwaji wa watu kwenye masuala nyeti yahusuyo nchi yao na wao wenyewe na ndiyo sababu mwaka jana ameanzisha jitihada za mchakato wa katiba ambapo wananchi watapata nafasi ya kushiriki moja kwa moja.

Mpango wa ubia wa uwazi serikalini ni mpango wenye Lengo la kuwapa wananchi nafasi ya kushiriki zaidi katika kuamua mambo yanayowahusu, kupitia vyama visivyo vya kiserikali na vya Kijamii.

Ubia huu unashirikisha kwa usawa wawakilishi wa Serikali kwa upande mmoja na wawakilishi wa Asasi zilizofikiwa za kiserikali kwa upande mwingine.

Nchi hamsini na tano (55) duniani zimejiunga na mpango huo hadi kufikia sasa kutoka nchi 8 mwaka jana ambapo mpango ulianza.

Kwa kujiunga katika mpango wa OPG, nchi hizi zinatarajiwa kubadili mwenendo wake wa kuendesha mambo yake ili uwe wa uwazi zaidi.

Marekani na Brazili ni wenyeviti wenza ambapo Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bibi Hilary Clinton amesema Marekani inaamini kuwa nchi iliyo kwenye mpango wa OPG itakuwa salama na ya amani zaidi ambapo ameisifu Tanzania kwa hatua mbalimbali ambazo imepiga katika kutekeleza mpango huu.

Pamoja na kikao cha OPG, Rais Kikwete amefanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Dilma Rousseff na Waziri Mkuu wa Georgia Bw. Nika Gilauri. Katika mazungumzo yao,  mahusiano ya nchi hizi na haja ya kuwepo ushirikiano wa karibu na   uwekezaji ni mambo yaliyopewa kipaumbele.

Pamoja na kutoa hotuba hiyo ya ufunguzi, leo Rais  Kikwete pia ametembelea taasisi ya utafiti  wa  Kilimo (Brazilian Agriculture Research Enterprise)  kwa kifupi  EMBRAPA ambapo  ameona technolojia  ya kisasa na utafiti unavyoendeshwa katika kituo hicho chenye vituo vingine mikoani vipatavyo 47.

Tayari kituo hicho kimeanza ushirikiano na Tanzania ambapo watanzania watakwenda kituoni hapo kwa ajili ya mafunzo  mwezi Juni mwaka huu.

Rais anaendelea na ziara yake ambapo tarehe 18 April, anatarajia kutembelea Makao Makuu ya World Food Program (WFP) na kuona juhudi zinazofanyika za kupambana na njaa.

Tarehe 19 April, Rais Kikwete anatarajia kumalizia ziara yake kwa kufungua mkutano wa wafanyabiashara wa Brazil na Tanzania wenye lengo la kuhamasisha makampuni zaidi kutoka Brazil  kuwekeza Tanzania.

Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi.
Brasilia, Brazil.
17 April, 2012

No comments: