Tangazo

April 24, 2013

UMATI yamtunuku Mama Kikwete Tuzo ya Heshima

Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo Mama Salma Kikweteakipokea tuzo maalum kutoka UMATI iliyokabidhiwa kwake na Makamu Mwenyekiti wa UMATI Taifa Ndugu Charles Mugondo kwa kutambua mchango wake mkubwa hususan kwenye elimu ya mtoto wa kike hapa nchini. Tuzo hiyo alikabidhiwa wakati wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya UMATI Taifa huko Ubungo Plaza tarehe 243.4.2013. Picha na John Lukuwi wa Maelezo

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipokea kadi yake ya maisha kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa UMATI Taifa Ndugu Charles Mugondo kwa kutambua mchango wake mkubwa kwa jamii kuhusu afya ya mama na mtoto hapa nchini.

Na Anna Nkinda  -Maelezo

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (pichani),  ametunukiwa tuzo ya  heshima na Chama cha uzazi na malezi bora Tanzania (UMATI)  kutokana na kazi anazozifanya za kutoa elimu kwa mtoto wa kike na kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinapungua hapa nchini.

Aidha Mama Kikwete pia amekabibidhiwa kadi namba moja ya kuwa mwanachama wa maisha wa UMATI.

Hafla hiyo ya kumkabidhi tuzo Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) imeenda sambamba na ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa siku mbili wa UMATI  unaofanyika katika hoteli ya Blue Pearl jijini Dar es Salaam .

Akikabidhi tuzo hiyo Makamu Mwenyekiti wa UMATI Charles Mugondo alisema kuwa wameamua kumpa tuzo hiyo ili kuonyesha kuwa ni mwenzao kutokana na kazi anazozifanya za kuisaidia jamii ya kitanzania.

“Tumeona umuhimu wa kazi unazozifanya, hivyo basi tumeamua kukupatia tuzo hii ambayo ni ushahidi tosha wa kuonyesha kuwa unawajali watoto wa kike nchini tunakupongeza kwa hilo na tunakuomba  uendelee zaidi kuwasaidia vijana hasa wasichana wa Tanzania,” alisema Mugondo.

Akiongea mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Mama Kikwete alishukuru na kusema kuwa hakutegemea kupewa tuzo lakini anaamini kuwa wameangalia vigezo vya utoaji wa tuzo na kuona kuwa anastahili  kupewa .

“Huwa napenda kunukuu maneno ya Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Nyumba tunayoishi ni moja hakuna haja ya kugombania fito hii inamaanisha kuwa kazi tunayoifanya ni moja hivyo basi tunakatikiwa kushirikiana ili tuweze kuwahudumia wananchi” , alisema Mama Kikwete.

UMATI  ni chimbuko la huduma ya uzazi wa mpango nchini  hususani katika huduma za afya ya uzazi na harakati za kumkomboa na kumwezesha mtoto wa kike ili aweze kujitambua na kujimudu  katika maisha yake.

No comments: