Tangazo

June 24, 2013

SHY-ROSE AKUNWA NA MISWADA BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI

 Katibu wa Wabunge wa Tanzania Katika Bunge la Afrika Mashariki, Shy-Rose Bhanji akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu miswada mbalimbali iliyojadiliwa na bunge hilo kwa kipindi cha  mwaka mmoja. Kushoto ni mbunge wa bunge hilo, Abdullah Mwinyi. (Picha zote na Habari Mseto Blog)
 Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdullah Mwinyi akizungumza na waandishi wa habari leo. Kulia ni Katibu wa wabunge wa Tanzania katika bunge hilo, Shy-Rose Bhanji.

DAR ES SALAAM, Tanzania

KATIBU wa Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki, Shy-Rose Bhanji, amejivunia harakati chanya alizoshiriki katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuanza kushiriki vikao vya bunge hilo Juni mwaka jana, huku akiielezea kuvutiwa na miswada miwili inayosubiri baraka za Marais wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Shy-Rose, alisema kuwa, yeye kama mbunge amejifunza mengi katika miezi 12 ya uwapo wake bungeni, huku akiitaja miswada hiyo kuwa ni sheria ya Udhibiti wa Uzito wa Magari Barabarani ‘Vehicle Load Contol Bill’ na Punguzo la Vituo vya Ukaguzi Mipakani ‘One Stop Border Posts Bill.’
                                                                                                                                                                                                                                               
Aliongeza kuwa, bunge hilo limeijadili kwa kina miswada hiyo, ambayo kwa sasa inasubiri maamuzi ya Marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, huku akitoa wito kwa wafanyabiashara kutumia fursa za Kijiografia za Afrika Mashariki ili kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Shy-Rose alisema kuwa, sheria hizo zitakuwa na tija kubwa kwa wananchi na mataifa yanayounda Jumuiya ya Afrika Mashariki, kutokana na ughali wa ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa sasa, lakini pia urasimu ulioshamiri katika vituo vingi vya ukaguzi wa abiria na mizigo mipakani kwa wanaotoka nchi moja kwenda nyingine.

“Uhai wa barabara zetu Afrika Mashariki unategemea matumizi sahihi, yanayozingatia uzito wa magari kwa barabara husika. ‘Vehicle Load Control Bill’ ina kila kanuni itakayowabana madereva kuhakikisha wanatumia barabara kwa uzito sahihi wa mzigo garini, ili kuzifanya zidumu kwa muda mrefu,” alisema Shy-Rose.

Aliongeza kuwa, mawasiliano ya barabara ndio mhimili wa maendeleo katika nchi yoyote na ili kudumisha barabara kuepuka ujenzi ghali wa mara kwa mara, sheria hiyo imependekeza uzito wa juu kabisa kwa magari yanayotumia barabara za Afrika Mashariki uwe ni tani 55 na sio zaidi.

Alifafanua kuwa, muswada huo umezingatia mambo mengi, hasa kutokana na ukweli kuwa kabla ya hapo kila nchi ilikuwa na sheria yake ya uzito wa juu zaidi barabarani, huku nchi nyingine za Afrika Mashariki zikiwa hazina sheria hiyo na kuruhusu magari kubeba uzito wowote na kupita barabara yoyote.

Kuhusu muswada wa ‘One Stop Border Posts Bill,’ Shy-Rose alisema kuwa, ni wazi kwamba jamii ya Wana-Afrika Mashariki, imechoshwa na urasimu mkubwa unaowakumba wanapohitaji kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine, unaosababishwa na uwingi wa vituo vya ukaguzi wa abiria na mizigo yao, hivyo muswada huyo ni tiba ya kero hiyo.

“Sheria hii ikipitishwa na kuridhiwa na Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, itamaliza hadha za usafiri zisizo za lazima, wanazokabiliana nazo wananchi, kiasi cha kuchelewesha safari zao na kjurudisha nyuma harakati chanya za kujiletea maendeleo yao na nchi zao kwa ujumla,” alisema Shy-Rose.

Kwa upande wake, Mbunge mwingine wa bunge hilo, Abdullah Mwinyi, alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki imejikita kujiletea maendeleo kupitia nyanja tofauti, zikiwamo za Forodha, Soko Huria na Sarafu ya pamoja, ambapo Bunge hilo limejadili mengi yaliyo bora kuhusu Forodha na sasa wanaingia katika Soko Huria.

“Soko Huria ndio kiini halisi cha mafanikio ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Dalili za mafanikio kupitia nyanja hiyo zimeanza kuonekana, ambapo bidhaa nyingi za Afrika Mashariki zilizokuwa zikiuzwa huko Afrika Magharibi, kwa sasa zinaingia rasmi kwenye mzunguko wa nchi wanachama wa Afrika Mashriki na kuchangia maendeleo ya pamoja,” alisema Mwinyi.

Aidha, Shy-Rose na Mwinyi wakatumia fursa hiyo kuwasilisha pole ya pamoja kati yao na wabunge wengine wa Bunge la Afrika Mashariki, kwa wahanga wa bomu jijini Arusha, ambako watu kadhaa walifariki dunia na wengine kujeruhiwa vibaya, huku wakilaani vikali shambulizi hilo lililoathiri watu wasio na hatia.

“Tunaviomba vyombo vya dola kuhakikisha vinatumia kila njia kuwanasa waliohusika na kuwawajibisha kwa mujibu wa sheria. Tunawaomba wana Arusha na atanzania kwa ujumla kudumisha amani, upendo, utulivu na mshikamano miongoni mwa Watanzania,” walisisitiza wabunge hao.

Kwa mujibu wa wabunge hao, vikao vijavyo vya bunge hilo vitafanyika kama ifuatavyo: Agosti 18 hadi 29, Oktoba 13 hadi 26 vikao vitakuwa jijini Arusha, huku Novemba 17 hadi Desemba 6 vikao vikiwa jijini Nairobi. Desemba 19 hadi 31, Januari 9 hadi Machi 22 na Mei 25 hadi Juni 6 mwakani vikao vyote vitafanyika jiji Arusha.

No comments: