Tangazo

October 15, 2014

MAAFISA MIPANGO WASHIRIKISHE MAKUNDI MAALUM UPANGAJI BAJETI - DED IKUNGI

DSC01247
Mkuu wa shule ya msingi Ikungi mchanganyiko wilaya ya Ikungi, Mwl. Olivary Kamilly, akitoa taarifa yake kwenye kilele cha mahafali ya 63 yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo kongwe iliyoanzishwa mwaka 1944.

Na Nathaniel Limu, Ikungi

MWENYEKITI wa halmashauri ya wilaya Ikungi mkoani SIngida, Celestine Yunde, amewaagiza maafisa mipango kushirikisha viongozi wa taasisi zenye mahitaji maalumu wakati wa kuandaa bajeti.

Mwenyekiti Yunde ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye mahafali ya 63 ya wahitimu wa darasa la saba shule ya msingi Ikungi mchanganyiko. Alisema hatua hiyo itawajengea mazingira mazuri maafisa kutambua ukubwa wa bajeti katika taasisi husika.

Akifafanua,Yunde alisema shule ya msingi Ikungi Mchanganyiko, ni taasisi maalum kwa madi kwamba inayo wanafunzi wenye ulemavu mbali mbali na wasio walemavu ambao baadhi wametoka nje ya mkoa.

“Wanafunzi wenye ulemavu mbali mbali , ni wanafunzi ambao mahitaji yao mengi ni ya gharama kubwa.Ukiachilia mbali gharama za nauli wanakotoka,karibu kila kundi lina mahitaji maalum na ni ghali", alifafanua Yunde.

Alisema wanafunzi hao walemavu wanaishi kwenye mabweni, mahitaji yao ni ya gharama kubwa na hivyo halmashauri inayo jukumu la kushirikisha viongozi wa shule hiyo,wakati wa kuandaa bajeti itakayokidhi mahitaji.
DSC01263
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi,Celestine Yunde, akizungumza kwenye mahafali ya 63 ya shule ya msingi Ikungi mchanganyiko yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo.

“Naahidi mwezi huu tarehe 29, nitaleta shuleni hapa madiwani wote wa halmashauri yetu. Nataka madiwani hawa waje wajionee wenyewe uhitaji mkubwa wa fedha kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa shule hii yenye walemavu mbalimbali, wengine wanaandikia miguu badala ya mikono”,alisema.

Katika hatua nyingine, mwenyekiti huyo aliupongeza uongozi wa shule hiyo kwa ubunifu wake uliopelekea shule kupewa kompyuta 10 na printa moja, na mamlaka ya mawasiliano Tanzania.
“Katika taarifa yenu, mmesema shule ilishiriki shindano lililoendeshwa na mamalaka ya mawasiliano Tanzania, na kati ya zaidi ya shule 3,000 nchini zilizoshoriki shindano hilo,ninyi ni miongoni mwa shule nne tu, zilizofanikiwa kushinda. Hongereni sana na hasa pongezi hizi zimwendee mkuu wa shule, Olivary Kamily”,alisema mwenyekiti huyo.

Kwa mujibu wa wakuu wa shule hiyo Kamilly, msaada huo wa kompyuta, unaambatana na kufungiwa mtandao wa huduma ya intaneti kwa mwaka mmoja. Pia itazinduliwa website ya shule.

Jumla ya wanafunzi 165 walioanza shule mwaka 2008, 85 wamehitimu kati yao wavulana 25 na wasichana 60.
DSC01266
Mgeni rasmi katika mahafali ya 63 ya shule ya msingi Ikungi mchanganyiko, Celestine Yunde, akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu wa darasa la saba (mwenye ulemavu wa macho).
DSC01273
Baadhi ya wahitimu wa darasa shule ya msingi Ikungi mchanganyiko wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida, wakiwa wamepozi na vyeti vyao vya kumaliza elimu ya msingi.
DSC01278
DSC01287
Baadhi ya wazazi wa wahitimu wa darasa la saba shule ya msingi Ikungi mchanganyiko,wakishiriki burudani na wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi.
DSC01300
Bango la shule ya msingi Ikungi mchanganyiko wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida.(Picha na Nthaniel Limu).

No comments: