Tangazo

October 13, 2014

SKYLIGHT BAND IMEBADILI SURA YA MUZIKI WA LAIVU

DSC_0009
Wamiliki wa Skylight Band Dk. Sebastian Ndege na Justine Ndege wakiwa kwenye moja ya show za vijana wao Skylight Band ndani ya kiota cha maraha Thai Village Masaki jijini Dar.

Na MOBlog Team

KAMA ni mpenzi wa muziki hutasita kukubaliana nami kwamba tangu Skylight Band iingie katika ulimwengu wa muziki wa laivu nchini hapa, kuna mambo mengi yamebadilika hasa namna ya kutoa burudani hiyo miongoni mwa bendi ambazo zilikuwapo au tuseme zipo hadi sasa.

Bendi hii ambayo ilianza 2011 imekuwa tishio kutokana na aina yake ya muziki wanayoipiga ya Afro Pop.

Hivi karibuni kutokana na mafanikio hayo yanayoonekana dhahiri hasa katika viwanja vya Thai Village na Escape One, Mo Blog ilipata nafasi ya kuzungumza na Mkurugenzi wa Skylight Band, Justine Ndege ambaye yeye na ndugu yake Dk Sebastian Ndege ndio wamiliki wa bendi hiyo.

Kwenye mazungumzo hayo na Zainul Mzige wa MOblog ilitaka kujua jinsi wazo la kuundwa kwa bendi hiyo lilivyofikiwa,uundaji wenyewe ulivyokuwa, mikakati ya kujitambulkisha na kujua hali ya baadaye ya bendi na changamoto zake.
DSC_0096
Wanamuziki wa Skylight Band wakitoa burudani kwa mashabiki wao kwenye uwanja wao wa nyumbani kiota cha Thai Village Masaki jijini Dar kila siku ya Ijumaa wanakuwa hapo kuanzia saa tatu usiku: Kutoka kushoto ni Joniko Flower, Mary Lucos, Sony Masamba, Aneth Kushaba AK47 na Sam Mapenzi wakiwajibika jukwaani.

MO BLOG : Naomba kabla ya kuanza kwa mazungumzo jitambulishe kwa wasomaji wetu.

SKYLIGHT: Mimi naitwa Justine Ndege ni mkurugenzi wa skylight band na Skylight entatainment. Skylight ni bendi ya ndugu wawili, Dk Sebastian Ndege na Justine Ndege na wote ni wakurugenzi; sisi ni kaka na mdogo.

MO BLOG :Unaweza kutuambia namna mlivyofikiria kuanzisha bendi hii?

SKYLIGHT: Wazo la kuanzishwa kwa Skylight Band lilifanyika wakati tukiwa katika burudani, mimi na ndugu yangu.Tukiwa tunakunywa na kuangalia mambo yanayoendelea pale.Katika mazungumzo tukasema kuna kitu kikubwa tunaweza kukifanya kuboresha mazingira kama haya badala ya kunywa na kuzungumza na marafiki pekee.
Katika mauzngumzo tukasema kwanini tusiwe na bendi ya kuburudisha.
DSC_0108
Sehemu ya wanamuziki wa Skylight Band wakitumbuiza mashabiki wao wakiongozwa na Meneja wa Bendi hiyo kutoka kulia ni Aneth Kushaba AK47, Digna Mbepera, Sony Masamba a.k.a Fally Ipupa wa bongo na Hashim Donode.

MO BLOG: Ilitokea tu wazo la kuwa na bendi au kuna kitu kiliwasukuma?

SKYLIGHT : Ni wazi kipo kitu kilichotusukuma ndio maana tukawaza. Tulitaka kubadili mambo katika burudani.Huko nyuma Dk Sebastian Ndege alikuwa anafanya mambo ya ushereheshaji yaani mc, alikuwa DJ na alikuwa na vifaa vya muziki.Tukasema basi hebu tujaribu .

MO BLOG: Mlipoamua kwamba tujaribu nini cha kwanza mlikifanya, mliitisha vyombo vya habari kama wengine wanavyofanya tunataka hiki?

SKYLIGHT: Ha ha ha unaenda kasi sana, hapana. kwanza lazima uwe na mtu ambaye unajua anaweza kutengeneza mambo fulani. Kwa hiyo mtu wa kwanza kabisa kumfikiria ambaye tulishawahi kufanyanaye kazi alikuwa ni Aneth Kushaba. Tukamwambia basi tukutane nyumbani kwa Dk Sebastian na akafanya hivyo. Ndio kusema Skylight iliundwa nyumbani kwa Dk . Sebastian Ndege mwaka 2011.

Pale Aneth alichukua jukumu la kukusanya.Tukasema hebu Aneth kusanya watu tuone kama inawezekana. Muziki wa kwanza muziki wa pili tukasema inawezekana. Tukasema twende kazini kuleta changamoto kwenye muziki wa laivu.
DSC_0116
MO BLOG :Naam mazoezi yamefanikiwa baada ya hapo burudani mliianzishia wapi?

SKYLIGHT: Tulifanya utafiti wa kutosha, tukajaribu kufuatilia ,tukachekecha kuona tutaanzia wapi, tukapata sehemu yetu ya kwanza ilikuwa Mafia Fishing Lounge. Tukaanza pale tukajaribu kuleta mashabiki, tukaweka strategy (mikakati) tofauti ya kujitangaza. Tukaweka matangazo katika maradio, kwenye mativii (televisheni) na kwenye Blogs. Kwa matangazo hayo, basi tunashukuru Mungu tulifika sehemu tukagundua kwamba watu wameanza kulewa muziki wa laivu na Skylight Band ni kitu gani.

MO BLOG: Inaonekana mambo yenu yanenda poa hamna shida yoyote ukiangalia jinsi watu wanavyowashabikia?

SKYLIGHT: Changamoto kiukweli zipo lakini mpaka leo tunamshukuru Mungu tumepata mashabiki kutoka sehemu mbalimbali.Kiukweli chalenge (changamoto) ni nyingi sana zikiwemo gharama za kuweka wasanii , kuwatunza, kuwapa mishahara kuwahudumia, lakini tunashukuru Mungu mambo yanaenda vizuri.

MO BLOG: Mambo gani hasa mmejifunza kama menejimenti toka muanze kutoa burudani 2011?

SKYLIGHT: Toka tumeanza kufanya burudani jambo zuri tumegundua kwamba mashabiki wanatoka sehemu mbalimbali kila mkoa, kila kata kila sehemu na uzuri ni kwamba unaweza kusikia jina kubwa la Skylight, lakini ukija kwenye shoo zetu ambazo tunazifanya kila Ijumaa na Jumapili za public (zisizobinafsi) kiingilio ni reasonable (kinachowezekana kwa nafasi yetu kiuchumi). Unaposogea unakuta kiingilio sh elfu 5 Thai village; unaposogea Escape One unakuta kiingilio sh elfu 7, yote hayo yanatokana na strategy (mkakati) yetu ya kuleta au kuweka mabadiliko au changamoto kwenye muziki wa laivu.
DSC_0244
Meneja wa Skylight Band Aneth Kushaba AK47 akiwajibika jukwaani.

MO BLOG: Kwanini mfikirie kwamba mkakati wenu ndio hasa unaoleta changamoto?

SKYLIGHT: Kwa sababu mpaka tunaanza kufanya muziki wa laivu na kuweka Skylight Band, muziki wa laivu ulikuwa kama umeanza kupwaya kidogo kwa Sio tunafikiria tunaona. Kuna mabadiliko mengi katika muziki wa laivu tuliyoyasababisha. Bendi nyingi sasa, mathalani zinatumia mitandao ya kijamii kujitangaza. Sisi tulianza na mkakati wa kujitangaza kwa kutumia mitandao ya kijamii, tukisema jamani kuna kitu kipya mtaani kuna bendi inaitwa Skylight. Tukatumia picha, tukatumia maelezo, tunaionesha jamii, nayo ikatukubali. Ndio maana sasa hivi unaona kweli bendi sasa zinatumia mitandao ya kijamii. Tunashukuru sana wadau wa mitandao ya jamii, tunashukuru MOBlog na Zainul Mzige Meneja Mwendeshaji wake, wametusaidia sana, tuna mshukuru Haki Ngowi, LeMUTUZ, Jestina George, Global Publishers, Jamii Forum, Michuzi blog, DJ Sek Blog, DJ Choka, Wavuti, Vijimambo, Sunday Shomari, Fullshwangwe, Deo Rweyunga, Harakati za Bongo, Josephat Lukaza, Kajunason Blog, Kamera yangu, Bukoba Wadau, Gsengo, Michuzijr, Lukwangule Blog na wengine wengi kwa kuhakikisha kwamba Skylight inapata jina na kufika hapa ilipo. Lakini pia tunawashukuru mashabiki wameipokea vizuri bendi na wameiweka Skylight juu.
MO BLOG: Wakati tunafikia mwisho wa mahojiano yetu unaweza kutudadavulia nini mipango yenu ya baadae?

SKYLIGHT: Plani zetu sisi ni kwenda zaidi, sasa hivi tunakwenda kimataifa tunatafuta masoko kimataifa kwa sababu tunaamini soko la nyumbani tumefanya tunachohitajika kufanya, japo yapo mengi tunayotakiwa kufanya.Kwa kuzingatia strategy yetu tunaamini kuna lengo tumelifikia kwa hiyo tunataka kwenda kimataifa.

MO BLOG: unaweza kutaja baadhi tu ya mafanikio hayo?

SKYLIGHT: Mengine tumeshasema kuhusu mashabiki kutukubali lakini ukienda katika medani ya muziki yenyewe mpaka sasa Skylight band imeshatengeneza nyimbo nane ambazo zinafiti albamu lakini zile ambazo zipo kwa umma sokoni ni nyimbo tano na video tano.

MO BLOG: Ningefurahi kama ungeliwatajia watu nyimbo hizo na zingine tatu zipo hatua gani?

SKYLIGHT: Nyimbo yetu ya kwanza inaitwa “WIVU ambayo ina audio na video , nyimbo yetu ya pili ni “NASAKA DOUGH” nayo ina video na audio nyimbo yetu ya tatu ni “CAROLINA” ina audio na video, nyimbo yetu ya nne ni “PASUA TWENDE” na nyimbo zote zinapatikana katika mtandao wa You Tube. Nyimbo yetu ya tano inaitwa “MAPENZI GANI” na ipo katika audio na sasa inatengenezewa video ambayo itakuja .
DSC_0231
Sehemu ya mashabiki wa Skylight Band wakicheza moja ya staili za bendi hiyo kwenye kiota cha maraha cha Thai Village Masaki jijini Dar ambapo kila Ijumaa bendi hiyo inatoa burudani kwa mashabiki wake.

MO BLOG: Pamoja na kwenda kimataifa nini kingine mmekifikiria huko mbeleni?

SKYLIGHT: Mipango yetu ya mbeleni ni kuhakikisha kwamba tunafanyakazi kwa kuangalia soko.Ila tunashukuru kwa Mungu ni kuwa mpaka sasa hivi strategy tulizozipanga zinaenda sawa tukimaliza ngwe ya kwanza tutaenda ngwe ya pili.

Projection (malengo) zetu ndani ya miaka mitano tunataka tuwe Afro Pop and Live Band, the best in Tanzania (bendi bora ya muziki wa laivu wa pop).Na hii inaonekana hata namna tunavyoingia kwenye tuzo mbalimbali. Kwa bahati nzuri au mbaya tumepata nomination (uteuzi) za mtu binafsi katika tournament za Kili Music na tuzo zingine. Tunaamini mwaka mmoja ujao tutaingia katika kategori kama bend.

MO BLOG: Unaweza kmunitajia idadi ya wanamuziki na kazi wanayoifanya katika Skylight band?

SKYLIGHT: Jumla wapo 16 na meneja wa bendi ni Aneth Kushaba. Safu ya waimbaji ni yeye Aneth Kushaba AK47, yupo Mary Lucos, Digna Mbepera, Joniko Flower, Sam Mapenzi, Sony Masamba a.k.a Fally Ipupa na Hashim Donode.

Kwenye vyombo wapo Idrisa (mpiga drum), Baraka (mpiga drum), Emma ( mpiga bass), Danny Ki (mpiga bass), Tophy (mpiga bass) Amos ( mpiga kinanda),Daudi (mpiga tumba), Joshua Ngoje (mpiga solo) na Allen Kisso Mundele (mpiga solo).

MO BLOG: Una neno la mwisho?

SKYLIGHT: Ninalo.Tunawashukuru mashabiki wetu wote, wadau, waandishi wa habari tunaomba waendelee kutusapoti Skylight Band.

No comments: