Tangazo

November 14, 2015

Manispaa la Ilala yakanusha kuhusu mfanyabiashara aliyekuwa anakamua matikiti maji jalalani katika soko la Buguruni

Na Mwandishi wetu – Maelezo

Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu picha inayomuonesha mfanyabiashara akikamua matikiti maji katika jalala lililoko Soko la Buguruni jijini Dar es Salaam iliyotolewa na gazeti moja  la kila siku la hapa nchini na kusambaa katika mitandao ya kijamii.

Maandishi ya picha hiyo yalisema Mfanyabiashara akikamua matikitimaji katika jalala lililoko Soko la Buguruni bila kujali maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu ambao hadi watu 53 wamepoteza maisha katika jiji la Dar es Salaam ukweli ni kwamba alikuwa anakamua matunda hayo kwa ajili ya kupata  mbegu za matikiti maji kwa ajili ya kuziuza.

Ufafanuzi huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Isaya Mngurumi wakati akijibu swali la Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) Jumanne Sagini alipouliza kuhusu usafi wa soko hilo.

Sajini aliuliza swali hilo wakati wa mkutano kati yake na watendaji wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam uliofanyika katika ukumbi wa Karimjee na kuhudhuriwa na waandishi wa habari.

Akitoa ufafanuzi huo Mngurumi alisema jana waliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala na kutembelea soko hilo ili kujionea  uhalisia wa jambo hilo baada ya kufika sokoni hapo waligundua  kijana ambaye picha yake ilitolewa na gazeti hilo alikuwa anakamua mbegu za matikiti kwa ajili ya kuziuza na siyo kwa matumizi mengine.

“Kilichoripotiwa katika gazeti hilo na picha kusambazwa katika mitandao ya kijamii siyo sahihi, vijana  wa soko hilo huwa wanakata matunda yaliyotupwa katika jalala hilo wanayaanika na kuuza mbegu katika soko la  Buguruni”, alifafanua.

Kwa upande wake Katibu Mkuu huyo aliwataka watendaji hao kuona  umuhimu  wa kujibu haraka na  kukanusha taarifa ambazo zinapotosha ukweli na kuchafua sura ya muonekano wa Tamisemi ili wananchi  wajue ukweli.

Wakati huo huo Sajini alitoa onyo kali kwa walimu wakuu kuacha mara moja tabia ya kupokea hela ili wawaandikishe watoto wa darasa la kwanza kwani kuanzia sasa elimu ni bure kwa shule za Msingi na Sekondari.

Katibu mkuu huyo alisema ameshapokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa kuna baadhi ya shule za jijini Dar es Salaam wazazi wanapoenda  kuandikisha watoto wa darasa la kwanza wanatoa fedha  ili watoto waweze kuandikishwa kitu ambacho siyo sahihi.

“Sielewi ni kwanini maafisa elimu wa wilaya hamuwachukulii hatua walimu wakuu wenye viburi ambao wanakiuka agizo la Mhe. Rais linalosema  elimu ya msingi hadi Sekondari ni bure na kuwachangisha wazazi”.

“Hao walimu wanaopinga agizo hilo ni kina nani na fedha hizo zinaingia katika  akaunti gani?  Nitawachukulia hatua wote watakaohusika  kwani michango hii ni kero kwa wazazi”,. alisisitiza Sajini

Alimalizia kwa kuhimiza  kuwa mtoto akienda kuandikishwa asitozwe kiasi chochote cha fedha ila jamii itashirikishwa katika shughuli za maendeleo ya shule na utaratibu wa michango ya jamii mwongozo wake utatolewa na michango hiyo haitamlenga mtoto.

No comments: