Tangazo

October 4, 2011

WAHARIRI 50 KUJADILI MBINU ZA KUTOKOMEZA VITENDO VYA UKATILI

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya

Wahariri wapatao 50  kesho Jumatano  Oktoba 05, watakutana  jijini Dar es Salaam kujadili  jinsi vyombo vya habari vinaweza kutoa mchango mkubwa zaidi kuchangia juhudi za taifa za  kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, wasichana na watoto.  

Wahariri  hao wanatarajiwa  kuanngalia ni mambo gani ambayo wao wenyewe na  vyombo vyao  vitaweza kufanya ili viongozi na  wananchi mijini na vijijini  wachukue hatua  kuepusha vitendo vya ukatili wa kijinsia visitokee katika maeneo yao.

Kadhalika  watajadili ni mikakati gani vyombo vya habari vinaweza kuweka ili  kuweza kuibua matukio ya vitendo vya ukatili  dhidi ya wanawake, wasichana na watoto ili huduma stahili  za kimatibabu, kisheria na  ushauri ziweze kutolewa kwa  waathika wa vitendo hivyo viovu.

Chama Cha Wanahabari Wanawake  (TAMWA) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya idadi ya watu (UNFPA) wameandaa  mkutano huo wa wahariri ikiwa ni  sehemu ya mwendelezo wa  kampeni ya kitaifa  kuzuia vitendo vya ukatili  wa kijinsia kwa sababu vitendo hivyo  vinarudisha nyuma maendeleo ya familia na  taifa.

Wahariri hao watakaokutana katika ofisi za TAMWA, Sinza Mori  kuanzia saa 4.30 asubuhi hadi saa saba mchana   watapata fursa pia ya  kupata taarifa kuhusu hali halisi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia  hapa nchini na jitihada kadhaa zinazochukuliwa kukabili tatizo hilo.fisi

Vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, wasichana na watoto ni pamoja na vipigo, ubakaji, ukeketaji, kudhulumu wajane hazi za mirathi, ndoa na mimba za utotoni na kutelekeza watoto kunakoongeza watoto kuishi mitaani.

Tunaamini kuwa vyombo vya habari vikitumika  ipasavyo  kufanya  tatafiti, kutangaza na kufuatilia hatua kwa hatua  kesi za matukio  ya ukatili dhidi ya makundi haya  wadau watachukua hatua stahiki kupunguza tatizo hilo.

Wadau wanapaswa  kufanya juhudi kubwa kuepusha ukatili wa kijinsia ni pamoja na  viongozi wa umma  wakiwepo wa  vitongoji, vijiji na mitaa, madiwani, wabunge, polisi, mahakama,  mashirika ya kijamii, madhehebu ya dini, wizara mbali mbali, wafadhili, waathirika na umma kwa ujumla wanawake na wanaume mijini na vijijini.

Tafiti zinaonesha kuwa ukatili wa kijinsia ni matokeo ya  kutokuwepo haki sawa katika jamii baina ya wanaume na wanawake na kwamba vitendo hivi vina madhara makubwa kwa afya na ustawi wa wanawake.
 
Imetolewa na:
Ananilea Nkya
Mkurugenzi Mtendaji

No comments: