Tangazo

November 1, 2011

UZURI NA UMAARUFU VINAMPONZA QUEEN AISHA 'AISHA MADINDA'

Afichua siri nzito ya maisha yake


Na Emmanuel Malima
 
LICHA ya kuaminika kuwa ndiye mcheza shoo wa kike aliyewahi kupata mafanikio na jina kubwa kuliko wacheza shoo wote, kuna vitu vibaya ambavyo vimekuwa vikilitia doa jina lake.

Sifa mbaya za umalaya, ulevi na utumiaji wa dawa za kulevya ndizo zinazomfanya aonekane mtu tofauti katika jamii, ingawa mwenyewe anasema kinachomponza ni uzuri na umaarufu wake.

Achilia mbali mvuto wa rangi na umbile lake alilonalo ambalo linaweza kumvutia mwanaume yeyote rijali, lakini pia ubunifu, kujituma na uwezo wake katika fani nzima ya kucheza shoo vinasemekana kwamba ndiyo siri ya mafanikio yake.

Huyu si mwingine ni mcheza shoo wa bendi ya Extra Bongo 'Wazee wa kujinafasi,' Aisha Mohamed Mbegu ukipenda muite Aisha Madinda au Queen Aisha kama mwenyewe anavyotaka aitwe kwa sasa.

Jina lake limekuwa likivuma mno kwa mema na mabaya. Amewahi kutajwa kuwa ndiye mcheza shoo mwenye mvuto zaidi hapa nchini lakini pia amewahi kutupiwa kashfa nyingi mbaya zisizostahili kusomeka katika jamii.

Lakini hii yote inatokana na nini?

"Najua kila binadamu ana makosa yake. Kuna wakati nafsi haiwezi kujizuia kufanya maovu lakini maovu huwa yanatokana na ushawishi.

"Sikufichi, ila, kilichoniponza mimi ni uzuri na umaarufu wangu. Yako mambo mengi yanayosemwa juu yangu lakini si yote yenye ukweli. Kuna mengine ni uongo na uzushi.

"Watu wananivumishia mara Aisha kafanya hivi, mara kafanye vile ili mradi tu wanakuwa na nia zao mbaya pengine kutokana na wivu na chuki. Isipokuwa ukweli ninao mimi mwenyewe," ndivyo alivyoanza kusema Aisha katika mahojiano maalumu na Mtanzania.

Aisha ambaye jina lake lilivuma mno wakati akiwa na bendi ya The African Stars 'Twangapepeta' kwa sasa hayuko tena na bendi hiyo inayomilikiwa na Asha Baraka, bali amehamia katika bendi inayokuja juu na kutishia amani bendi nyingine za muziki wa dansi, Extra Bongo 'Wazee wa kujinafasi, inayongozwa na Ally Choki.

Katika mahojiano hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Meeda, ulioko Sinza Mori ambako Extra Bongo hutumbuiza kila siku za Jumamosi kama ukumbi wake wa nyumbani, Aisha 'kufunguka' kuhusu maisha yake binafsi, nini anachofanya pamoja na mipango yake ya baadaye.

Anasisitiza kuwa shutuma anazopewa nyingi zinapikwa na watu wasiomtakia mema ingawa masuala hayo anamuachia Mwenyezi Mungu.

"Aah, namuachia Mungu tu. Najua binadamu hawaachi kuongea. Walinisingizia mengi hadi kuna wakati nikajikuta natumbukia kwenye mambo yasiyofaa," anasema.

Kucheza kwake shoo ni uhuni?

Hata hivyo anasema anaithamini sana kazi yake ya ucheza shoo ambayo ndiyo inayomuendeshea maisha yake na kumfanya afike hapo alipo.

Anasisitiza kuwa kazi hiyo si uhuni kama ambavyo watu wamekuwa wakiidhania, bali uhuni hutokana an nafsi na mawazo ya mtu mwenyewe.

"Napenda tu kuwaambia watu wenye mtizamo wa namna hiyo kwamba kucheza shoo si uhuni bali ni tabia mtu kwa sababu kuna watu wengine ambao si wacheza shoo lakini ni wahuni kutokana na nafsi zao tu.

"Kwa ufupi uhuni, umalaya au wizi na tabia zingine zote mbaya kwenye jamii zinatokana tu na tabia ya mtu binafsi na sio kwa sababu eti fulani anacheza shoo.

"Wapenzi wa muziki hasa wa dansi wanapotuona sisi wacheza shoo wasitufikirie vibaya waone tuko kazini kwenye sanaa ambayo ndiyo fani yetu kama kazi nyingine yoyote.

Dawa za kulevya na picha za uchi?

Kuhusu shutuma mbalimbali zinazomzunguka kama vile matumizi ya dawa za kulevya, upigaji wa picha za uchi Aisha anasema hapendi kuzungumzia masuala hayo ila ni miongoni mwa matukio ambayo yanamuumiza mno katika maisha yake.

"Najisikia vibaya mno, kuna mtu asiyenitakia mema ambaye amekuwa akinivumishia mambo mabaya kwa faida yake mwenyewe. Kuna wakati alitengeneza picha za mtu anayefanana na mimi na kuvumisha kwamba yule ni mimi.

"Ni kitu ambacho nilikuwa sikukutegemea maishani mwangu. Ilikuwa ngumu hata kuamini kama mtu anaweza kufanya vitu kama vile.

"Aliyefanya vile alikuwa na nia ya kutaka kuniharibia jina na sifa mbele ya jamii na hata kwenye familia yangu na hivyo kunimaliza kisanii.

"Inaniuma na kunisikitisha sana. Sitokaa nisahay tukio lile katika maisha yangu. Hata hivyo ninafurahi kwamba baadaye ilikuja kubainika kuwa aliyepiga picha za uchi siyo mimi ni msichana mwingine aliyefanana na mimi.

"Msichana yule alinisaidia zaidi alipoelezea jinsi picha zile zilivyopatikana. Hata mimi pia nilimsikitikia kwani nasikia alikuwa ni mchumba wa mtu na kwamba eti picha zile alizipiga akiwa na rafiki zake lakini kwa bahati mbaya simu yake iliyokuwa na picha zile ikapotea na ndipo aliyeipata hiyo simu ndio akaamua kuzisambaza kwa kutumia jina langu. Bado sijajua ni kwa nini," anasema Aisha.

Anasisitiza kuwa jambo la msingi ni kujifunza watu wanaweza kumchafua kwa lengo la kumharibia jina kutokana na chuki tu.

"Tukio lile limenifundisha mengi, nimejua kwamba kuna watu wanaweza kukuharibia mambo yako bila sababu. Watu wa aina hii wanapaswa kuepukwa," anasema.

Aidha anatoa ushauri kwa watu wengine kuepukana na kutokupiga picha za ovyo na kuepukana na kamera kwani mtu hawezi kujua picha hizo zinaweza kukuharibia kiasi gani.

"Yako mambo mengi yanayoweza kutokea kwa sababu kama yaliweza kumtokea yule siwezi kujua hata mimi au wewe iko siku yanaweza kunikuta hivyo ni bora kuepukana na vitu kama hivyo."

"Kwangu mimi nimekwishasema kwamba kuna faida na hasara ya kuwa mtu maarufu na matokeo yake ndiyo yale.
'Kwa sisi watu maarufu, viko vitu vingi sana vinavyoweza kutupata viwe ni vizuri au vibaya. Na umaarufu unatofautiana hasa kwa sisi wasanii tunaofanya kazi ya muziki.

"Unaweza kufanyiwa mambo mazuri hadi ukafurahi, laikini pia unaweza kufanyiwa mambo mabaya au kusingiziwa mambo ambayo sio ya kweli kabisa kama hilo la picha za uchi," anasisitiza.

Kuhusu utumiaji wa dawa za kulevya, Aisha hataki kuligusia hilo zaidi ya kusisitiza kwamba kwa sasa anakunywa na kuvuta tu.
"Zamani nilikuwa sinywi ka
bisa pombe, lakini kwa sasa nakunywa na kuna wakati navuta kwa sababu ya kutuliza mawazo.

"Nilianza kunywa na kuvuta ili kutuliza kichwa changu ambacho kilikuwa na mambo mengi yanayonichanganya. Polepole nikajikuta nikizoea na kuzoea ingawa sasa niko katika mapambano ya kujaribu kuacha kabisa ili nirejee na kuwa Aisha mwingine kabisa aliyebadilika kimaisha.

"Hata mimi inanisikitisha sana kusikia habari kwamba eti mimi ni teja. Hii ndiyo hasara ya umaarufu ambayo nimekuwa nikiisema."

Kuhusu wanaume wanaomsumbua?

Aisha anakiri kuwa kutokana na asili ya kazi yake ya ucheza shoo na uzuri alionao, mara nyingi amekuwa akikumbana na usumbufu mkubwa kutoka kwa wanaume wakware wanaojaribu kumshawishi au kuwataka kimapenzi.

"Hili mbona liko wazi, kila tunapofanya shoo ni lazima tukutane na watu wa aina hii. Lakini kwa kifupi tu ni kwamba ninapokuwa stejini huwa niko kazini kama mtu mwingine anayekuwa kazini kwake.

"Ninapotoka pale huwa nimechoka na ninachotakiwa kukifanya ni kwenda nyumbani kupumzika tu basi, usumbufu mwingine sipendi.

"Kama mtu unaamua kujiheshimu inabidi iwe hivyo ili kujiepusha na vishawishi. Tamaa siku zote huwa ni mwanzo wa kuangamia."

Aliondokaje kwa 'dada' Asha Baraka?
Kwa miaka mingi Aisha alizoeleka kuwa ndiye nembo ya shoo katika bendi ya Twangapepeta, ambayo ni mali ya mwanamama Asha Baraka.

Mbali na kuwa nembo ya Twanga kwa muda mrefu, lakini pia alikuwa ni 'shosti' mkubwa wa Asha Baraka, kutokana na ukweli kwamba wao walikuwa kama ndugu kwa vile wanatoka mkoa mmoja wa Kigoma.

Cha kushangaza ni kwamba Aisha hivi karibuni aliamua kumtosa 'dada' yake huyo na kuhamia Extra Bongo kwa Choki.

Anafafanua kuwa kilichomsukuma kuhamia Extra Bongo ni si kingine zaidi ya kutaka kujiendeleza kimuziki.
"Nilipokuwa Twanga ni kama nilikuwa nimefungwa minyororo na sasa nimeikata.

"Ukweli ni kwamba, kukaa sehemu moja inachosha na unaweza kujikuta ukishindwa kuongeza ubunifu kwa sababu utajiona uko sawa wakati wote.

"Lakini unapotoka na kwenda sehemu nyingine ndipo unapoweza kukabiliana na changamoto mbalimbali na kujifunza mambo mengi.

"Mimi binafsi niliona Choki anakuja juu na anapata mafanikio hivyo sikusita kumuunga mkono. Naona fahari sana kuwa naye hapa.

"Kitu kizuri zaidi ninachokifurahia hapa Extra Bongo ni kwamba wanamuziki tuko huru sana, kila mmoja anathaminiwa na kusikilizwa. Na hata mtu akitaka kutoa mawazo yake yanasikilizwa na kama ni shida inatatuliwa mara moja.

"Nafurahia sana maisha hapa Extra Bongo na kusema kweli nafurahia kuwa na watu kama kina Choki, Roggart Hegga, Ferguson, Super Nyamwela, Danger Boy na wengineon ambao tulikuwa nao Twangapepeta."

Anasema tangu atue katika bendi hiyo amekuwa akifurahia shoo zao zote kutokana na ukweli kwamba bendi yao kwa sasa imekubalika na imepokelewa vizuri na mashabiki kutokana na jinsi 'inavyokimbiza' sokoni.
Anakumbuka jinsi alivyopokelewa vizuri tangu siku ya kwanza alipotambulishwa kwa mashabiki ambao walimbeba na kumtuza pesa kibao.

"Nilitamani kulia kwa sababu nilikumbuka kuna wakati tuliwahi kwenda jijini Amsterdam Uholanzi ambako nako mashabiki walinipokea kwa furaha kama vile."
 
Ni kipaji au mazoezi?

Wacheza shoo wako wengi lakini ni kwa nini jina la Aisha ndilo liwe juu zaidi kuliko wengine licha ya kuwa umri wake unazidi kusogea?

Akifafanua kuhusu hili, Aisha anasema ana nyota kali ya kupendwa lakini kikubwa alichonacho ni kipaji alichozaliwa nacho.

"Namshukuru Mungu kwamba alinipa kipaji, kipaji ambacho anakiendeleza vizuri. Kama nisingekuwa na kipaji hata ningefanya vipi mazoezi nisingeeleweka.

'Nimekiendeleza kipaji changu kwa muda mrefu hadi sasa umri naona unazidi kwenda ingawa nyota yangu haijashuka.

"Isipokuwa kitu kimoja tu ninachokiamini kwamba iko siku nitalazimika kustaafu kazi hii ili kuwapisha wengine."

"Ninatarajia nitakapostaafu niendelee na masuala ya biashara. Inategemeana na jinsi mambo yatakavyokuwa.

Nafikiria pia kuanzisha shule ya unenguaji ambayo itakuwa ikiwafundisha wasanii wachanga wanaopenda kazi hii. Hii nadhani itatoa fursa nzuri kwa wengine kufuata nyayo zangu.

"Bado nina muda wa kutosha kuendelea kucheza shoo, muda utakapofika nitaamua kustaafu kwa uamuzi wangu mwenyewe na pia ni kwa sababu najua kabisa hata hivi leo kwamba uchezaji shoo una mwisho wake.

"Najua siwezi kucheza shoo hadi uzeeni. Nimeshajipangia kwamba nitakapofikisha umri fulani nitaachana na mambo ya muziki na kuwapisha wengine.

"Labda ninachoweza kufanya ni kuendelea na uimbaji, nimejifunza tayari kuimba."

"Ninapenda sana kuimba na nitafurahi kwa sasa nikiwa nafanya vitu vyote viwili kabla ya kustaafu, yaani naimba na kucheza.

Huyu ndiye Queen Aisha ambaye jina lake kamili ni Mwanaisha Mohamed Mbegu ingawa alizoeleka zaidi kwa jina la Aisha Madinda.

Ingawa alizaliwa Mei 5, mwaka 1979 jijini Dar-es-salaam lakini ni mwenyeji wa mkoa wa Kigoma ambako pia ndiko aliposoma katika shule ya Msingi Kiganamo kabla ya kurejea tena jijini Dar es Salaam na kuanza shughuli za muziki.

Aisha hajaolewa ingawa ana watoto wawili Side na Naomi.


 

No comments: