Meneja Maendeleo ya Biashara wa Auric Air, Deepesh Gupta (kushoto) akikabidhi msaada wa fulana kwa Mratibu wa mashindano ya mbio za Tabora Livingstone Marathon, Ramadhani Makula jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Uratibu wa mbio hizo, Tullo Chambo.
****************************************** Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Ndege ya Auric Air ya jijini Dar es Salaam imejitosa kusapoti mashindano ya Mbio ya Tabora Livingstone Marathon yanayotarajiwa kufanyika mjini Tabora Machi mwakani.
Mbio hizo za kwanza katika historia ya Mkoa wa Tabora, zitakuwa za Nusu Marathon Kilomita 21 na zile za kujifurahisha za Kilomita 5.
Akikabidhi msaada wa fulana kwa Mratibu wa mbio hizo, Ramadhani Makula jijini Dar es Salaam jana, Meneja Maendeleo ya Biashara wa Auric Air, Deepesh Gupta, alisema, wamesukumwa kutoa msaada hyo ili kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu nne chini ya Rais Jakaya Kikwete katika kuendeleza na kuhamasisha michezo hapa nchini.
Gupta alisema, kwa kuzingatia malengo na madhumuni yam bio hizo, wameona japo watoe msaada huo mdogo wa fulana zitakazotumiwa na waratibu na wasimamizi wa mbio hizo ili kusaidia kufanikisha tukio hilo muhimu.
Akipokea msaada huo, Mratibu wa Tabora Livingstone Marathon, Makula, aliishukuru kampuni hiyo na kutoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuwaunga mkono katika kufanikisha mbio hizo za kihistoria.
Makula alisema, hafla ya uzinduzi rasmi wa mbio hizo ambao utawashirikisha wadau na wafadhili mbalimbali utafanyika jijini Dar es Salaam Januari 10.
Aliwataka vijana wenye vipaji mbalimbali wa Mkoa wa Tabora na maeneo ya jirani kujiandaa na mbio hizo, huku akitoa pongezi kwa ushirikiano unaotolewa na Chama cha Riadha Mkoa wa Tabora.
|
No comments:
Post a Comment