Tangazo

February 13, 2012

Nneka afanya shoo Sauti za Busara 2012

Mwimbaji wa Nigeria, Nneka Egbuna amefanya shoo ya aina yake na ya kihistoria katika tamasha la tisa la busara.

Shoo yake ya jana imefunga pazia ya ziara yake katika Ukanda wa Afrika Mashariki iliyodhaminiwa na Goethe Institute. Shoo nyingine amezifanya katika nchi  za Kenya, Rwanda, Uganda  na  Zanzibar.

Nneka aliimba nyimbo kutoka katika albamu yake mpya aliyoiachia mwaka jana iitwayo ‘ Soul is Heavy’. Ilimchukua miaka mitatu kuandika na kurekodi  albamu hiyo yenye nyimbo kumi na tano ambazo zilichujwa kutoka katika nyimbo hamsini alizoandika.

Mwaka 2005, aliachia albamu yake ya kwanza iitwayo ‘ Victim Of Truth’, na kufuatiwa na No Longer At Easy iliyotoka  (2008). Mwanamuziki wa Marekani,  Lenny Kravitz alivutiwa naye na kumchagua kuwa mwimbaji msaidizi katika ziara yake huko Marekani.

Akiwa na Kravitz ndipo alipoandika ‘Soul is Heavy’.Wakati wa shoo yake ndani ya Ngome Kongwe aliimba nyimbo mbalimbali za mapenzi na machungu ambazo zipo katika mahadhi ya  reggae, hip-hop, R&B na vintage soul.  

Alikuwa akiimba huku akiwasaidiwa na Garry Sullivan kutoka Marekani  ( Drums), Emmanuel  Ngolle  Pohossi kutoka Cameroon ( Bass),  Jonas ‘Mo’ Da Silva Pinheiro  kutoka Brazil ( Guitar) na Nis Goetting kutoka Germany (keyboard).

Alielezea kuwa rushwa ni ugonjwa wa kijamii ambao ulikuwa ukipigwa vita na marehemu Fela Anikulapo Kuti ambaye pia alikuwa akitokea Nigeria.

Anasema rushwa inaathari kubwa kwa bara la Afrika huku akitolea mfano Niger Delta alikozaliwa na kukulia.
 
Baada ya kusalimia wakazi wa Zanzibar aliimba wimbo maarufu wa ‘ V.I.P. (Vagabond In Power)’ ambao uliripua kelele za furaha na kuimba pamoja   ‘Vagabond in power (Vagabond in power o!)’.

Baada ya kumaliza shoo mashabiki hawakutaka ashuke jukwaani waliomba aendelee kuwaburudisha. Uimbaji wake na ujumbe alioubeba umedhihirisha kuwa muziki unatumia lugha ambayo inaweza kufikisha ujumbe kirahisi zaidi.

No comments: