Mchungaji Jean Uwinkindi |
Mtuhuhumiwa wa mauaji ya kimbari ambaye yuko mikononi mwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya kimbari ya Rwanda (ICTR), Mchungaji Jean Uwinkindi atahamishiwa nchini Rwanda kabla ya Aprili 19, 2012.
Aprili 5, 2012, Rais wa ICTR, Jaji Vagn Joensen, aliamuru kwamba Uwinkindi ahamishiwe Rwanda ‘’katika kipindi cha siku 14 kutoka tarehe ya amri hiyo’’ na kumwelekeza Msajili ‘’kufanya taratibu zote zinazohitajika kwa ajili ya kutekeleza amri hiyo.’’
‘’Rais anamwelekeza Msajili kuanza mara moja majadiliano na Rwanda kujua nini cha muhimu kufanyika ili kutekeleza uhamisho wa Jean Uwinkindi,’’ inasomeka sehemu ya uamuzi huo.
Kwa mujibu wa uamuzi huo, Rais pia amemwelekeza Msajili wa mahakama hiyo kuwateua wanasheria wa ICTR kwa kushauriana na yeye ili kuwa ‘’wasimamizi wa muda’’ wa kesi hiyo pindi Uwinkindi atakapohamishiwa nchini Rwanda na hadi hapo Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR) au chombo kingine kitakapoteuliwa rasmi kuwa msimamizi wa usikilizaji wa mwenendo wa kesi ya Uwindikindi.
Juni 28, 2011, ICTR ilipitisha uamuzi wa kuhamishia kesi ya Uwinkindi nchini Rwanda na uamuzi huo kuthibitishwa na Mahakama ya Rufaa Desemba 16, 2011.
Kesi nyingine mbili pia zimeamriwa kupelekwa nchini Rwanda ambazo zinawahusu watuhumia wawili ambao bado wanasakwa na mahakama hiyo.Watuhumia hao ni pamoja na Fulgence Kayishema na Charles Sikubwabo.
Pia Aprili 12, 2012, ICTR itasikiliza maombi mengine ya mwendesha mashitaka kutaka kesi ya mtuhumiwa mwingine wa mauaji hayo, Bernard Munyagishari, kwenda kusikilizwa nchini Rwanda.
Mchungaji Uwinkindi anashitakiwa kwa mauaji ya kimbari na kuteketeza kizazi.
No comments:
Post a Comment